Lauwo aondolewa kesi ya Aveva, Hanspoppe

Muktasari:

Septemba 14 mwaka huu, Takukuru ilitangaza kuwasaka Hans Poppe na mkandarasi Franklin Lauwo ili kuunganishwa katika kesi ya utakatishaji fedha inayowashilishilia kina Aveva.

Dar Es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemuondolea shtaka, Mfanyabiashara Franklin Lauwo katika kesi inayowakabili viongozi wa Klabu ya Simba.

Uamuzi huo, umetolewa leo, Oktoba 19, 2018 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba baada ya upande wa mashtaka kushindwa kupata.

Lauwo alikuwa anakabiliwa na shtaka la kuendesha shughuli za ukandarasi bila kuwa na leseni kupitia Kampuni yake ya Ranky ambayo haijasajiliwa na Bodi ya Wakandarasi.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro akisaidiana na Mutalemwa Kishenyi, amedai kuwa Lauwo bado hajajisalimisha katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

"Lauwo alikuwa ajisalimishe leo hii Takukuru, lakini mpaka sasa ameshindwa kufanya hivyo na nimewasiliana na wenzetu wa Takukuru asubuhi hii, wameniambia bado hajajisalimisha," amedai Kimaro na kuongeza

"Hivyo chini ya kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Makosa ya Jinai, tunaomba Mahakama yako kumuondoa katika hati ya mashtaka hii, ili kesi iweze kuendelea."amedai.

Kimaro baada ya kueleza hayo, Hakimu Simba aliondoa shtaka hilo.

"Mahakama imeondoa mashtaka ya Lauwo, kama walivyoomba upande wa mashtaka, hivyo kupitia kifungo hicho, mahakama itawasomea maelezo ya awali, washtakiwa watatu ambao wapo Mahakamani hapa," alisema Hakimu Simba.

Katika kesi hiyo, Viongozi wa Klabu ya Simba wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Aliyekuwa Rais wa Klabu hiyo, Evans Aveva, Makamu wake Godfrey Nyange na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu ya Simba, Zacharia Hanspoppe.

Miongoni mwa mashtaka yanayowakabili ni pamoja matumizi mabaya ya madaraka kwa kuhamisha fedha za Klabu bila idhini ya Kamati ya Utendaji ya Simba, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uwongo na mashtaka ya utakatishaji fedha yanayowakabili Aveva na Kaburu.