LAMATA: Afunguka kutofanya kazi na Wema, Uwoya

KATIKA sehemu iliyopita tuliona jinsi mwongozaji wa filamu, Leah Mwendamseka a.k.a Lamata, akielezea sababu za kuvutiwa na ‘mahendsamu boi’ na wanawake warembo katika kuwapa dili katika kazi zake za sanaa anazoandaa akisema jambo hilo linachangia kuvutia watazamaji huku pia akisisitiza hapotezei wenye vipaji. Endelea…

UNAMJUA MSUMBUFU WA KAPUNI?

Anasema katika tamthiliya hiyo wasanii ambao wanasumbua wanapokuwa wanarekodi ni binamu yake Diamond Platnumz, Romy Jons ambaye ndani humo anaigiza kwa jina la ‘Jordan’ na Paul, jambo ambalo linawafanya wapoteze muda mwingi.

“Kama kuna kipengele ambacho Jordan au Paul wanarekodi lazima uwe makini maana kutokana na ucheshi wao muda mwingi huwa wana kazi ya kuchekesha tu, sasa kama hauko makini mnaweza kutumia muda mwingi kurekodi sehemu inayowahusu wao tu,” anasema Lamata.

Akimzungumzia Jordan ambaye ni msanii mpya lakini anafanya vizuri kwenye tasnia hiyo, ndiye alimtengeneza hadi akafikia alipo sasa.

MKALI WA KUNASA VITU

Lamata anaweka wazi kati ya wasanii anaofanya nao kazi kila mmoja ana uwezo wake katika kuelewa, lakini amejisifu kuwa anapomfundisha mtu lazima ashike.

“Najiona mwenye bahati kwani kila ninayefanya naye kazi huwa anashika ingawa katika maisha yote watu huwa wanatofautiana. Msanii ambaye ana uwezo wa kushika mambo kwa haraka zaidi ya wengine ni Mama Mjata (Thecla) unapomwelekeza kazi haichukui muda kunasa,” anasema Lamata.

THAMANI YA TASNIA YA FILAMU

Tasnia ya filamu ni kama ipo kwenye changamoto kutokana na watu kuwa kama wameisahau. Kila mtu anazungumza lake, wengi humtaja Steven Kanumba ambaye ni marehemu kuwa kufariki kwake dunia na tasnia hiyo ikapoteza mvuto.

“Ni kweli kwa sababu hakuna kitu kipya, watu wamechoka na hadithi kama zinarudiwa. Mtu akitaka kurudisha filamu kwenye chati lazima afanye kazi ya ziada, namaanisha aumize kichwa kutunga hadithi nzuri itakayotingisha kwa ubora,” anasema Lamata ambaye pia amepanga kufanya mapinduzi kwenye kazi hiyo.

“Mbali na Kijiji cha Lamata, mapinduzi niliyopanga ni kutunga hadithi nzuri zaidi zitakazowavuta watu. Mfano Kapuni nataka iwe mfano mtu akiingalia asichoke, ukirudia na kufanya ujanja ujanja unawachosha watazamaji kisha wanaachana nayo.”

Anafafanua watu wamekimbilia tamthiliya kwa sababu inalipa inapokubalika, lakini filamu fupifupi za kwenye CD haziwalipi, masilahi wanayopata yanakuwa madogo.

“Hata zile nchi zilizoendelea kwenye tasnia ya filamu kazi wanazofanya ni kutengeneza tamthiliya na hata televisheni zinafanya hivyo, kukuta hadithi fupi kama zamani ni nadra.”

WEMA, UWOYA

Katika kazi zake, Lamata amekuwa akitumia wasanii tofauti hasa Gabo, Mwanaheri, Jacqueline Wolper, Kajala na Odama huku wasanii wengine wakubwa kama Wema Sepetu na Irene Uwoya akiwaweka kando.

“Si kama sipendi kufanya kazi na Wema au Uwoya ni majukumu tu, kama utafika wakati wa kufanya kazi nao nitafanya. Kwangu hakuna msanii mkubwa, anayefanya vizuri katika kazi husika ndiye mkali, lakini si kwa sababu ya majina,” anasema Lamata.

PACHA WAMVURUGA, JINA LAMATA

Huwezi kuamini kitu ambacho kilikuwa kinamsumbua Lamata alipokuwa mdogo na historia ya jina ambalo anatumia la Lamata.

“Wakati nikiwa mdogo sikuwahi kuwaona mapacha, sasa mahali tunaishi kota kulikuwa na pacha na wao walikuwa wakubwa kwangu. Siku ambayo niliwaona kwa mara ya kwanza nilipata wakati mgumu, yaani niliona kama vituko au watu wasio kawaida halafu nikawa nawaogopa sana,” anasema Lamata.

“Sasa walipojua nawaogopa wakatumia udhaifu huo kunitisha na mambo mengine na kilichokuja kutokea baadaye, wakawa marafiki zangu.”

Anasema katika hao pacha mmoja alikuwa anaitwa Lamra na Lamata. Lamata ndiye alikuja kuwa rafiki yake wa karibu zaidi.

“Kwa sababu alikuwa karibu na historia yake namna ilivyo, ndio maana nikajipa jina hilo la Lamata kwenye kazi zangu,” anafafanua.

PESA YA KWANZA

Lamata anasema alianza kazi hiyo akijitolea kwa takribani miaka mitatu, mwaka 2012 walipotoa Filamu ya ‘My Princess’ ambayo ilimpa pesa na kubadilisha sehemu kubwa ya maisha yake.

“Katika filamu hiyo ndio nilianza kupata maisha, mwanzo tulikuwa tunapata asante tu zilitusaidia kwenye nauli na mambo mengine. Nakumbuka niliitumia pesa hiyo kwa kununua gari aina ya Toyota Fan Cargo na nyingine nilipeleka kanisani fungu la kumi,” anasema Lamata ambaye ni muumini wa Kanisa la Lutherani na filamu hiyo alikuwa mwongozaji, msanii akiwa Wolper na wengine.

“Baada ya hapo nami nikawa nakaa mezani na kujadili biashara na watu namna gani tutalipana na baadaye kuanzisha kampuni yangu ya Lamata.”

RATIBA YAKE KWA SIKU

“Starehe yangu ya kwanza ni movie, hivyo huwa naamka saa 11, alfajiri kila siku kwa ajili ya kuangalia filamu tofauti, achana na ile ya saa 8:00 usiku ninayoamka kwa ajili ya kujifunza. Ninapoamka alfajiri ya saa 11 natumia saa tano hadi saa 4:00 asubuhi namaliza kuangalia,” anasema Lamata ambaye anaweka wazi hatumii kilevi ndio maana anapenda soda aina ya Fanta.

Anasema baada ya hapo ndipo anaandaa chai, anakunywa na kuendelea na mambo mengine ya kazi zake pamoja na kuweka sawa msosi wa chakula cha mchana na usiku.

Imeandikwa na Doris Maliyaga, Charity James na Rhobi Chacha