LA Galaxy yamtwangia Messi simu yamuita Marekani fasta

Muktasari:

Tangu atibuane na Mkurugenzi wa Michezo wa Barcelona, Eric Abidal, Messi amekuwa akihusishwa na kuondoka bure Nou Camp huku klabu kadhaa zikitajwa kuwania saini yake wakati wa kiangazi.

LA Galaxy imeingia kwenye vita ya kuisaka saini ya nahodha wa Barcelona, Lionel Messi na tayari timu hiyo inadaiwa kumpigia simu na kumuita Marekani staa huyo pindi dirisha la usajili la majira ya kiangazi litakapofunguliwa.

Tangu atibuane na Mkurugenzi wa Michezo wa Barcelona, Eric Abidal, Messi amekuwa akihusishwa na kuondoka bure Nou Camp huku klabu kadhaa zikitajwa kuwania saini yake wakati wa kiangazi.

Inaelezwa LA Galaxy ambayo imewahi kuwatoa Ulaya mastaa kama Ashley Cole, Steven Gerrard, David Beckham na Zlatan Ibrahimovic imeamua kumfuata Messi, huku ikidaiwa kuwapigia simu wawakilishi wake kuangalia uwezekano wa kupata huduma ya staa huyo. Inadaiwa viongozi wa LA Galaxy walimpigia simu baba mzazi wa Messi, baada ya kuondoka kwa Zlatan kumuuliza kama mwanawe yuko tayari kutua Marekani.