Kwisha! Makambo apata mbabe Bara

Muktasari:

Ambundo amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Januari wa Ligi Kuu Tanzania (TPL) msimu wa 2018/2019 baada ya kuwashinda Ayoub Lyanga wa Coastal Union ya Tanga na kipa Juma Kaseja wa KMC ya Dar es Salaam, aliyoingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa na Kamati ya Tuzo ya TPL inayotolewa na TFF.

STAA wa Yanga, Herritier Makambo sasa amepata kiboko yake wa tuzo za mchezaji bora wa mwezi kutoka timu ya Alliance, anayejulikana kwa jina la Dickson Ambundo.

Makambo aliwaburuza wachezaji wazawa kwa kuchukua tuzo ya mchezaji bora mara mbili mfululizo ya mwezi Novemba na Desemba kabla ya Ambundo naye kubeba.

Ambundo amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Januari wa Ligi Kuu Tanzania (TPL) msimu wa 2018/2019 baada ya kuwashinda Ayoub Lyanga wa Coastal Union ya Tanga na kipa Juma Kaseja wa KMC ya Dar es Salaam, aliyoingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa na Kamati ya Tuzo ya TPL inayotolewa na TFF.

Kwa mwezi huo wa Januari, Alliance ilicheza michezo mitano, ambapo Ambundo alitoa mchango mkubwa kwa timu yake kupata pointi 11 ikishinda michezo mitatu na kutoka sare miwili, huku akifunga mabao matatu na timu hiyo kupanda kutoka nafasi ya 17 hadi ya tisa katika msimamo wa ligi.

Kwa upande wa Kaseja alikuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya timu ya KMC kwa mwezi huo, ambapo timu yake ilicheza michezo minne ikishinda yote na kujikusanyia pointi 12 na kupanda kutoka nafasi ya 10 hadi ya tatu, ambapo Kaseja aliruhusu bao katika mchezo mmoja dhidi ya Coastal Union ambao KMC ilishinda mabao 5-2.

Wakati Lyanga alionesha uwezo mkubwa katika michezo ya Coastal Union na kuwa tumaini katika ufungaji ikiwa ni pamoja na kupachika nyavuni mabao matatu.

Pia Kamati y, imemchagua Kocha wa KMC, Etienne Ndayiragije kuwa Kocha Bora wa mwezi Januari akiwashinda Malale Hamsini (Alliance) na Amri Said (Biashara United).

Ndayiragije aliiongoza timu yake katika michezo minne, ambayo ilishinda michezo yote na kuvuna pointi 12 na kupanda kutoka nafasi ya 10 hadi ya tatu katika msimamo wa ligi.

Kwa upande wa Malale aliiongoza timu yake katika michezo mitano ikishinda mitatu na kutoka sare miwili ikipanda kutoka nafasi ya 17 hadi ya tisa katika msimamo, wakati Amri Said kwa mwezi huo timu yake ilicheza michezo sita, ikishinda mitatu, sare mmoj na kupoteza miwili hivyo kupanda kutoka nafasi ya 20 hadi ya 18 katika msimamo.

TFF ina utaratibu wa kuwazadia wachezaji bora wa kila mwezi, huku pia mwisho wa msimu kukiwa na tuzo mbalimbali zinazohusu ligi hiyo, ambapo msimu wa mwaka 2017/2018 tuzo 16 zilitolewa kwa washindi wa kategori mbalimbali.

Washindi wengine waliowahi kubeba tuzo hiyo msimu huu ni Meddie Kagere wa Simba (Agosti), Eliud Ambokile wa Mbeya City (Septemba), Emmanuel Okwi wa Simba (Oktoba), mwezi Novemba na Desemba alishinda Heritier Makambo wa Yanga.

Kwa upande wa makocha waliowahui kubeba tuzo ni Amri Said wakati huo akiwa Mbao FC (Agosti), Mwinyi Zahera wa Yanga (Septemba, Novemba na Desemba), Hans Pluijm wa Azam (Oktoba).