Kwanini huyu Amunike apewe muda Stars

Friday September 14 2018

 

By MWALIMU KASHASHA

NI wakati wa wapenzi na wakereketwa wa soka hapa nyumbani kuanza kujenga utamaduni wa kuwa na subira pamoja na uvumilivu wa kutosha ili kumpa nafasi mwalimu mpya wa timu yetu ya taifa wa sasa na wengineo watakaofuata kwa lengo kuu moja tu, la kuwaruhusu kufanya kazi inayosababisha wapewe kandarasi hapa kwetu.

Subira,utulivu na uvumilivu miongoni mwa mashabiki na wapenzi wa soka itawasaidia makocha kufanya kazi kwa utulivu mkubwa wa akili na mwili ili watupatie kile walichonacho.

Ni takribani mwezi mmoja na zaidi sasa tangu shirikisho la soka Tanzania (TFF) limtangaze mkuu mpya wa benchi la ufundi la timu za taifa za Tanzania (kuanzia Taifa Stars hadi Serengeti Boys) kutoka nchini Nigeria, mwalimu Emmanuel Amunike, aliyechukua mikoba ya mwalimu mzawa, Salumu Mayanga.

Mantiki kubwa iliyoko nyuma ya mabadiliko haya ya hiari,kiufundi na ya makusudi kabisa ni kutokana nia njema na thabiti ya TFF na Watanzania kwa ujumla kutaka kuona mapinduzi na mabadiliko chanya ambayo ni endelevu ya kiwango bora cha soka cha timu ya taifa na maendeleo ya mpira kwa mapana yake hapa nchini.

Kwa hakika uamuzi huu ni matokeo ya kilio na maono ya wapenzi wa soka walio wengi kwa muda mrefu kutokana na ukweli kwamba mwendo wetu ama kasi yetu bado si ya kuridhisha, tukijilinganisha na majirani zetu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kati na licha ya mataifa mengine yaliyoko eneo la Maziwa Makuu, kuzidi kutuacha na kuweka pengo kati yetu na wao kwenye soka katika ngazi ya klabu na timu za taifa, pamoja na kwamba kwa nyakati tofauti tumekuwa tukipanda na kushuka.

Kwa akili ya kawaida na lugha nyepesi sana, watanzania kwa ujumla wetu tunapenda sana soka lakini ni kama vile mchezo wenyewe hautupendi, na ni kweli soka halitupendi?

Siamini katika hili, lakini kuna mahali tunakosea, na kama tunakosea bado hatujaweza kubaini ni wapi tunakosea? Itakuwa ni jambo la ajabu kama mpaka leo hatujui udhaifu wetu kiasi kwamba bado tupo kwenye nafasi za mwisho mwisho kwenye viwango vya soka duniani.

Lazima tukubali kwamba tunakosea mambo fulani fulani katika mfumo mzima wa kuendesha soka, kwa vyovyote vile yapo mazuri sana yanayofanyika lakini pia upungufu mwingi unaosababisha kupwaya kwenye mzunguko mzima wa sayansi ya kuendesha soka kitaalamu.

Miongoni mwa matatizo ya muda mrefu katika soka la Tanzania ni waalimu kufanya kazi kwa shinikizo kutoka kwa baadhi ya viongozi, wapenzi na mashabiki bila kufuata utaratibu maalumu wa namna ya kufikisha hisia, mawazo na maoni yao kwa mwalimu au viongozi.

Ualimu kama taaluma nyingine yoyote ni kazi inayozingatia kanuni na taratibu lakini pia ualimu wa mpira una miiko na maadili yake na hapa ndipo tatizo la waalimu wengi wanaofanya kazi hususani katika ngazi ya timu ya taifa na klabu za Ligi Kuu na Daraja la Kwanza wanaposhindwa kutumia vizuri taaluma yao kwa kuwa wanakutana na mitihani na vikwazo vingi vya kuingiliwa katika kufanya uamuzi kwa mujibu wa taaluma, weledi na utashi wao, mwisho wa siku wanatupiwa lawama kwamba hawana uwezo wa kufundisha soka.

Katika mazingira ya namna hii, mwalimu yeyote yule aliyesomea taaluma ya ualimu wa soka akahitimu na akaelimika vizuri na kuanza kazi akiamini katika kile alichofundishwa na waalimu wake tena waliobobea na wenye sifa zinazotokana na misingi ya tafsiri ya mchezo huu kwa mujibu wa shirikisho la soka Kimataifa (Fifa) na asili ya mchezo wenyewe, lazima hatakubali kuendeshwa ama kuingiliwa katika taaluma yake. Kimsingi haya yapo yanalalamikiwa na waalimu wa hapa nyumbani na hata wa kigeni,lazima tubadilike.

Haiwezekani tuwe na utamaduni wa kubadilisha walimu miaka nenda rudi wakati hatupati mafanikio ya kutosha. Tunatakiwa kujiuliza swali moja kubwa na kufanya ulinganifu (comperative study) na mataifa mengine. Je? kwa kubadilisha walimu mara kwa mara hususani miaka ya hivi karibuni kumetusaidia kupata mafanikio yapi? Wengi tunakumbuka uwepo wa mwalimu Marcio Maximo katika timu ya taifa kwa miaka minne mfululizo alitusaidia kusogea angalau nafasi za juu kidogo, tulikuwa miongoni mwa nchi mia moja bora,lakini tangu aondoke tunazidi kurudi nyuma, hapa kuna kitu cha kujifunza.

Tukiwa tunapigana kufa na kupona kujaribu kupata nafasi ya kucheza fainali za Afcon nchini Cameroon mwaka ujao 2019, timu yetu ta taifa bado hatuna uhakika wa kufanya hivyo mpaka sasa katika kundi letu la L lenye timu za Uganda, Cape Verde na Lesotho.

Hesabu za yamkini haziwezi sana kutusaidia kwenda kwenye fainali kwani kila timu inapiga hesabu hizo hizo, njia pekee kwa jinsi kundi hili lilivyo ni kushinda michezo yetu yote iliyobaki bila kujali tunacheza wapi ( ugenini au nyumbani ),katika mpira wa kisasa popote pale ushindi unaweza kupatikana.

Mwishoni mwa juma lililopita Watanzania tuliishuhudia Taifa Stars ikivaana na Uganda “ The Cranes” mchezo uliomalizika kwa sare ya bila kufungana, katika pambano la kuwania kufuzu fainali za Afcon. Haikuwa kazi rahisi, kwa ujumla ni matokeo ya faraja kwa wapenzi wa soka kwani the cranes ni miongoni mwa timu bora na ngumu kwa sasa barani Afrika.

Kwa takwimu na kumbukumbu za jumla, huu ulikuwa ni mchezo wa 54 kwa timu hizi kukutana, Uganda wameshinda mara 29,Tanzania mara 10 na hii ilikuwa ni sare ya 15.

Sote tunafahamu kwamba huu ulikuwa ni mchezo wa kwanza kwa kocha mpya kuongoza kikosi cha Stars katika mchezo mkubwa, mgumu na wa mashindano.

Kwa bahati mbaya mwalimu ameanza kibarua chake kwa kukumbana na changamoto katika mpira wa hapa nyumbani ya kuwakosa baadhi ya nyota waliokuwa ni chaguo lake la kwanza kutokana na uzembe mkubwa wa wao wenyewe ama wa waajiri wao (klabu ), na kusababisha kuchelewa kuripoti kambini.

Lakini kwa ujasiri mkubwa na taaluma yake haraka alifanya uamuzi wa kuwaita wachezaji wengine kikosini ambao hakika hawakutuangusha ,kazi walioyoifanya huko Uganda ilikuwa ya kutosha.

Kwa muda mrefu tumekuwa na kasumba na mazoea ya ovyo, kwamba wachezaji wa timu ya taifa lazima watoke timu za Simba na Yanga, inawezeka zipo sababu za msingi na za kiufundi, lakini kama tukijipanga vizuri kwa kuweka mipango na mikakati ya kutosha, siyo lazima timu ya taifa iundwe na wachezaji wengi wa simba na yanga.

Nampongeza sana mwalimu Amunike kwa kuchukua hatua stahiki ya kuwatimua nyota waliochelewa kuripoti kambini. Tukumbuke kwamba huyu ni mgeni, ana malengo yake kama mtaalamu, ana falsafa zake katika kufundisha soka,lakini pia ametoka katika taifa la mpira kwa maana ya mafanikio anafahamu njia walizopitia huko kwao hadi kuwa taifa kubwa katika soka.

Uzoefu wake kama mchezaji wa kariba hiyo na baadaye kuwa kocha anaweza kuwa msaada mkubwa sana katika maendeleo ya mpira wa Tanzania endapo tutampa ushirikiano wa kutosha na tukaacha kuishi kwenye mpira kwa mazoea.

Kitendo cha kuwafukuza wachezaji wanaofikirika kuwa wapo kwenye kiwango bora kwa sasa bila kujali matokeo yangekuwa nini huko Uganda ni meseji ya kutosha kwamba anaijua kazi yake na ana msimamo.

Kufuzu Afcon au Kombe la Dunia siyo lele mama, tunahitaji kufanya kazi ya ziada na kuwekeza vya kutosha, kwa bahati nzuri idadi ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje imeongezeka, hivyo mchanganyiko wa vipaji na uzoefu katika timu yetu ya taifa ni mkubwa. Amunike awafuatilie wachezaji kwa karibu na kuwaona ili awe na wigo mpana wa kuchagua, upo uwezekano wa kufuzu Afcon 2019. Ni mechi nne tu.

Advertisement