Kwako Kashasha: Burundi wameisaidia Stars kiufundi

TIMU ya taifa ‘Taifa Stars’, Jumapili iliyopita ilicheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Burundi na kupoteza kwa bao 1-0, mechi iliyochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Bao hilo pekee la Burundi katika mchezo ule lilifungwa na mshambuliaji Saido Ntibazonkiza katika dakika ya 85 ambao hapana shaka umewafanya walipe kisasi cha kutolewa na Stars kwa mikwaju ya penalti 3-0 katika hatua ya awali ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2022 zitakazochezwa Qatar, baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi mbili zilichezwa nyumbani na ugenini kwa kila moja.

Kwa ujumla ilikuwa ni jambo jema kwa Stars kupata mchezo huo ambao ulichezwa kwa mujibu wa kalenda ya mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (Fifa).

Pengine tunaweza kufikiria meci haikuwa sahihi kwa sababu ya nafasi ambayo Burundi wapo katika FIFA Rankings ambapo Tanzania tuko juu yao, wao wakiwa katika nafasi ya 149 wakati sisi tupo kwenye nafasi ya 134.

Lakini hata hivyo Burundi waliweza kutupa changamoto za kiufundi ambazo zitalisaidia benchi la ufundi la Stars chini ya Kocha Etienne Ndayiragije katika maandalizi ya timu hiyo kwa ajili ya mechi mbili za kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) dhidi ya Tunisia ambayo itachezwa mwezi ujao.

Katika mchezo ule, Taifa Stars tulikuwa wazuri katika safu ya ulinzi na kiungo. Tulicheza vyema hasa katika first half ambayo Burundi walianza kwa staili ya kujilinda.

Tatizo kubwa ambalo tulikuwa nalo katika mchezo ule ni katika eneo la mwisho ambalo ni safu ya ushambuliaji, tulipata nafasi kadhaa ambazo tulishindwa kuzitumia.

Mbwana Samatta alijitahidi ku-drive lakini alichungwa mno na mabeki na viungo wa Burundi. Tusingetarajia acheze huru kwani wanamfahamu kuwa ni mchezaji wa daraja la juu ambaye ukimpa nafasi anaweza akakuadhibu.

Saimon Msuva naye alijaribu kupambana lakini changamoto ikawa ni huduma ambayo alikuwa akipata. Tulitumia mfumo wa 4-3-3 ambao unategemea washambuliaji wawili kufanya movement lakini walijikuta wakipata mipira migumu na hakukuwa na zile penetration passes.

Tulichojifunza ni kwamba huu ndio muda muafaka wa kuandaa washambuliaji. Inawezekana wachezaji kutokuwa pamoja kwa muda mrefu kulisababisha mwalimu kutopata nafasi ya kuwashape washambuliaji wake kwa ajili ya mchezo ule.

Wale Burundi walikuwa wazuri zaidi kwenye matumizi ya nguvu. Kulikuwa na utofauti mkubwa wa fitness baina yao na sisi na kuna wakati refa alilazimika kupuliza filimbi kutokana na wachezaji wao kutumia nguvu kubwa pindi walipokuwa wakigombea mipira na wachezaji wetu.

Lakini pia walionekana bora kwenye eneo la mwisho . Walikuwa na ubunifu. Walitengeneza nafasi chache ambazo zilikuwa za hatari na nyingine kama sio uhodari wa kipa David Kisu katika kuziokoa, pengine tungeweza kufungwa mabao mengine zaidi ya lile moja.

Bao walilotufunga linatukumbusha kwamba tunapaswa kuongeza umakini pindi tunaposhambuliwa.Mfungaji alipopokea mpira, walinzi walifikiri angesogea tena mbele na ule mpira lakini yeye aliamua kuupiga na ukaenda nyavuni.

Kwa ujumla kama tunataka kusonga mbele tunatakiwa kwa kiasi kikubwa kutatua udhaifu wa safu ya ushambuliaji ambayo ndio inaonekana kufanya makosa mengi.

Maeneo mengine hayana tatizo sana lakini tatizo la upande wa ushambuliaji tuna kazi kubwa ya kufanya.

Kimsingi ni jambo la kupongeza kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuwezesha Taifa Stars kupata mchezo ule dhidi ya Burundi kwani ni mechi ambayo mwalimu alitaka anataka kuangalia ile tunaita transition movement.

Hii ni namna timu inavyoweza kureact pale tunapokuwa na mpira na pale tunapoupoteza.

Pamoja na hayo, mwalimu na makocha wenzake wamepata fursa ya kuwatazama baadhi ya wachezaji ambao awali hawakupata nafasi ya kuwemo katika kikosi hicho ama kwa sababu za kiufundi au majeruhi lakini pia inatoa mwanya kwa walio nje ya kikosi kuitwa siku za usoni kwa ajili ya kuimarisha katika nafasi ambazo zimeonyesha udhaifu.

Kwa hiyo kupitia mechi ile, benchi la ufundi la Taifa Stars bila shaka limeshafahamu yapi ya kuyafanyia kazi na kuyarekebisha kwa ajili ya mechi zetu mbili muhimu, kubwa na ngumu zinazofuata dhidi ya Tunisia ambazo zitacheza kati ya Novemba 13 hadi 17 mwaka huu.

Hapana shaka TFF itaendelea kuipatia idadi kubwa ya mechi za kirafiki timu zetu za taifa hapa nchini ili kutoa nafasi kwa makocha kufahamu madhaifu na uimara wa kiufundi ili waweze kurekebisha au kuboresha zaidi.