Kwaheri Norwich City

Muktasari:

Norwich imecheza mechi 35 na kukusanya alama 21, ambapo hata ikiwa itashinda michezo yake mitatu iliyosalia itakuwa imefikisha alama 30 ambazo hazitamfanya kutoka kwenye mstari wa kushuka daraja.

LONDON, ENGLAND. LIGI Kuu England imeendelea jana Jumamosi ambapo michezo mitano ilipigwa na kushuhudiwa Norwich City ikiaga rasmi ligi hiyo baada ya kupigwa mabao 4-0 na West Ham United.

Norwich imecheza mechi 35 na kukusanya alama 21, ambapo hata ikiwa itashinda michezo yake mitatu iliyosalia itakuwa imefikisha alama 30 ambazo hazitamfanya kutoka kwenye mstari wa kushuka daraja.

Mchezo mwingine ulikuwa kati ya Watford ambayo imezidi kujiondoa kwenye mstari mwekundu wa kushuka daraja baada ya kuichapa Newcastle United mabao 2-1 na kufikisha alama 34 baada ya kucheza mechi 35 na kushika nafasi ya 17, mbele ya AFC Bournemourth ambayo inashika nafasi ya 18 kwa alama 28 baada ya kucheza mechi 34.

Mabingwa wa ligi hiyo, Liverpool waliendelea kupata matokeo mabaya tokea watangazwe rasmi kuwa mabingwa baada ya kutoa sare ya bao 1-1 na Burnley ikiwa Anfield.

Chelsea waliendelea na kupokea kipigo baada ya kukubali kichapo cha bao 3-0 dhidi ya Sheffield United, kipigo hicho kimeifanya kuwa kwenye hatari ya kutomaliza nafasi nne  za juu.

Chelsea imebaki na alama 60, baada ya kucheza mechi 35, wakati Leicester City ina alama 59 baada ya kucheza mechi 34, huku United ikifuatia na pointi 58, ikiwa imecheza mechi 34. Hivyo ikiwa United na Leicester watashinda michezo yao inayofuata watamshusha hadi nafasi ya tano.

FT Brighton & Hove Albion wakiwa nyumbani walifungwa bao 5-0 na Manchester City ambao wameokana kuimarika zaidi siku za karibuni.

Ligi hiyo itaendelea tena leo Jumapili kutakuwa na michezo minne, Wolverhampton Wanderers watakuwa na kibarua mbele ya Everton mchezo utapigwa saa 8:00 mchana.

Aston Villa wakikipiga dhidi ya Crystal Palace majira ya 10:15 mchana, Tottenham Hotspur Studium patakuwa na shughuli pevu kati ya Arsenal na Tottenhm Hotspurs mchezo ambao utapigwa saa12:30 jioni.

Spurs inaingia katika mchezo huo ikiwa inashika nafasi ya 10 na alama 49, huku Arsenal yenyewe ikiwa nafasi ya nane na alama 50 baada ya wote kuwa wamecheza mechi 34.

Mchezo wa mwisho utakuwa kati ya AFC Bournemouth ambao wapo kwenye hatari ya kushuka daraja wakiwa  nafasi ya 18 na alama 28 watakapowaalika Leicester City saa 3:00 usiku.