Kwa hawa jamaa vunja kibubu

Wednesday March 25 2020

 janga la virusi vya Corona,Ligi Daraja la Kwanza ,Namungo FC,Lipuli FC,Mwanasport,

 

By Thomas Ng'itu

LIGI imebakiza mechi 10 kumalizika na kwa sasa imesimama kutokana na janga la virusi vya Corona, huku cha kushangaza klabu nyingi za Bongo zinautumia muda huu kujipanga upya kwa msimu ujao.

Mwanaspoti limeangazia washambuliaji ambao wamefanya na wanaendelea kufanya vizuri msimu huu, huku kukiwa na ugumu wa kuendelea kusalia katika vikosi vyao kwa msimu ujao;

RELIANTS LUSAJO

Ameshaini sana mpaka sasa. Lusajo aliwahi kusajiliwa na Yanga lakini baada ya kujiona hana nafasi alitimkia zake Arusha kujiendeleza kielimu, kabla ya kurejea msimu uliopita kwa kucheza Ligi Daraja la Kwanza akiwa na Namungo na kuipandisha.

Msimu huu yeye ndio kinara wa mabao katika klabu hiyo akiifungia mabao 11 mpaka hivi sasa huku akiwa mguu ndani mguu nje kuendelea kusalia katika kikosi hicho na ni wazi uamuzi wa kusalia ni mdogo sana ingawa wasimamizi wake wanasema lolote linaweza kutokea. Anawindwa na Simba na Yanga.

PAUL NONGA

Advertisement

Umri wake ni miaka 32 kwa sasa lakini amewaonyesha wachezaji vijana bado ni mpambanaji anapokuwa uwanjani.

Nonga ameifungia Lipuli mabao 11 sawa na Lusajo wa Namungo, pia amekuwa bora katika timu zote alizopita ikiwemo Mwadui.

Kuna uwezekano Nonga akaota mbawa Lipuli haswa kutokana na hali ngumu ya kiuchumi ndani ya timu hiyo.

YUSUPH MHILU

Hakukata tamaa hata pale alipotolewa kwa mkopo msimu uliopita na kwenda zake Ndanda kwani ni kama ndio ilimuaminisha anaweza kucheza kokote pale.

Yanga walimvunjia mkataba na msimu huu alisaini mwaka mmoja kuichezea Kagera Sugar na mpaka sasa tayari ana mabao 11 na uwezo wake wa kucheza kama winga na mshambuliaji wa kati umemuongezea soko.

DARUWESHI SALIBOKO

Ana miaka 21 na huu ndio msimu wake wa kwanza kwenye ligi, anapata maujuzi sana kwa mkongwe kama Paul Nonga pale Lipuli. Ametupia mabao manane mpaka sasa, lakini silaha yake kubwa ni umri wake na kipaji chake ambacho timu zinamwona kama hazina.

AYOUB LYANGA

Ana mabao saba. Msimu uliopita alikuwa anahitajika na Yanga lakini ishu ya mkataba ikawa ni kizuizi kwake na dili hilo likashindikana.

Hajakata tamaa na msimu huu ameendelea kufanya vizuri akiwa na Coastal Union.

WAZIRI JUNIOR

Hakuwa bora Azam FC kutokana na majeraha. Msimu huu ni kama amekubali kuanza upya kwani alitimkia Mbao FC na kucheza soka akiwa huru na ameonyesha uwezo baada ya kufunga mabao saba licha kushindwa kuisaidia Mbao iliyonasa kwenye eneo la kushuka daraja, lakini yamempa soko na huenda akapata ulaji.

Advertisement