Kwa Simba hii, Kununa uwe na sababu

KAMA ni sifa, basi hao Simba wamezidi sasa na kama ni kuwakera wapinzani wao, basi wanawakeraa kweli. Ndio, achana na mechi yao usiku wa jana wakati wakimkaribisha jijini Dar es Salaam Kocha Mwinyi Zahera na chama lake la Gwambina, unaambiwa kikosi cha Kocha Sven Vandenbroeck ni moto ile mbaya hasa safu yake ya mbele.

Washambuliaji wanne wa Simba wameonyesha kuwa na makali yanayofanana, licha ya utofauti wa muda ambao kila mmoja anapewa kucheza kikosini.

Nahodha John Bocco, Chris Mugalu, Charles Ilanfya na Meddie Kagere licha ya kutokuwepo na aliyewahi kucheza kwa dakika 90 angalau katika mechi tatu kati ya saba zilizopita ambazo timu hiyo imecheza tangu msimu huu ulipoanza, wameonyesha njaa ya kufumania nyavu tofauti na matarajio ya wengi.

Wanne hao kila mmoja ameonyesha kutumia vyema muda anaopewa kuwemo kikosini, kupachika mabao ambayo hapana shaka yanazidi kuliweka katika wakati mgumu benchi la ufundi la Simba katika upangaji wa kikosi.

Japo nahodha Bocco ndiye anayeonekana kuwa kipaumbele cha Kocha Sven, Ilanfya, Mugalu na Kagere ambao wamekuwa hawapati muda mwingi wa kucheza, bado wameonekana kula naye sahani moja kutokana na takwimu nzuri za ufungaji walizonazo licha ya muda mfupi wanaopata.

Katika mechi saba ambazo Simba imecheza dhidi ya Vital’O, Namungo FC, AFC, Ihefu, Mtibwa, Biashara United na African Lyon, Bocco amecheza nne kati ya hizo kwa dakika 308 na akafanikiwa kupachika mabao matatu.

Mabao hayo ni moja moja katika mechi ya kilele cha Tamasha la Simba dhidi ya Vital’O ya Burundi, lingine akipachika katika mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Namungo huku moja akifunga katika mechi ya ufunguzi wa ligi dhidi ya Ihefu.

Hata hivyo, Bocco hakufunga katika mechi ya raundi ya pili ya Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar ingawa alicheza kwa dakika 90.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Bocco, Mugalu ndiye anaonekana kuwa tishio zaidi kwani kicha ya kucheza mechi tatu tu kwa dakika chache, amekuwa na takwimu bora za ufungaji kulinganisha na wengine.

Mugalu aliyesajiliwa na Simba akitokea Lusaka Dynamos ya Zambia, amecheza mechi tatu tu za Simba kwa dakika 134, lakini ameweza kufunga mabao matatu. Mechi hizo pekee alizocheza Mugalu amefunga dhidi ya Vital’O, Biashara United na ya kirafiki dhidi ya African Lyon.

Mshambuliaji ambaye anafuatia kwa kupewa muda mwingi wa kucheza nyuma ya Bocco, Meddie Kagere naye amekuwa hafanyi makosa pindi anapopata fursa kwani yeye hadi sasa ameifungia Simba mabao matatu katika mechi tano alizocheza kati ya saba.

Kagere ambaye amecheza mechi tano kati ya hizo saba, amefunga mabao yake matatu dhidi ya Biashara United na mawili dhidi ya AFC na jumla ya dakika alizocheza ni 211.

Nyuma ya watatu hao, nyota aliyesajiliwa kutoka KMC, Charles Ilanfya amekuwa hayuko nyuma kwa kufumania nyavu, ingawa ndiye mchezaji aliyecheza idadi ndogo ya mechi na dakika kati ya hao wanne.

Ilanfya amecheza mechi tatu za Simba kwa dakika zisizozidi 120, lakini amepachika mabao mawili na mechi hizo ambazo alifanikiwa kufumania nyavu ni dhidi ya Viatl’O na ile dhidi ya African Lyon, zote zikiwa ni za kirafiki.

Makali hayo ya washambuliaji hao wanne wa Simba, yameonekana kuwagawa wadau wengi wa soka juu ya nani apaewe nafasi ya kuanza na hata mfumo gani bora wa kutumika ili kuweza kuwapa fursa ya kucheza, ugumu ambao hata benchi la ufundi la Simba limekiri kuupata katika upangaji wa kikosi.

“Kikubwa nafurahishwa na wanachokifanya kwa sababu kila mmoja anatumia vizuri nafasi anayopewa jambo ambalo ndilo nahitaji kuliona kwao ingawa inaleta changamoto kidogo katika upangaji wa kikosi japo mwisho wa siku yule aliyefanya vyema mazoezini na anaonekana anaendana na mahitaji ya timu kwa mechi husika ndiye atakayepata nafasi,” alisema Kocha Sven.

“Timu inatakiwa kuwa hivi na sio kumtegemea mchezaji mmoja ambaye siku akidhibitiwa au akiwa hayuko sawa, mnapata wakati mgumu,” aliongeza kocha huyo raia wa Ubelgiji.

Kocha wa Pamba na mshambuliaji wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe alisema kinachofanywa na mastraika hao wa Simba ndio jambo sahihi.

“Sio vibaya timu kuwa na idadi kubw aya washambuliaji wazuri. Hiyo inaongeza chachu na ushindani kwa kila mmoja na kumfanya ajitume ili amshawishi kocha ampe nafasi ya kucheza.

Naamini hawa washambuliaji wataisaidia sana Simba kutokana na huo ushindani na ufanisi wao uwanjani,” alisema Mwakingwe.