Kwa Mugalu, pasi kisigino bao

Muktasari:

Simba imeshinda 2-0 dhidi ya African Lyon kwenye mchezo wa kirafiki uliopigwa katika Uwanja wa Chamazi Complex

KIKOSI cha klabu ya Simba kimeshinda 2-0 katika mchezo wa kirafiki dhidi ya African Lyon uliochezwa katika uwanja wa Chamazi leo Septemba 22.

Magoli ya Chris Mugalu na Charles Ilanfya katika kipindi cha pili yalifanya kurahisisha kazi baada ya kipindi cha kwanza timu zote kutoka 0-0.

Klabu ya African Lyon katika mchezo huo waliweza kuendana na kasi ya Simba katika dakika 45 za kipindi cha kwanza.

Katika kipindi cha pili Simba walionekana kuhitaji goli la kuongoza na dakika 47 Chris Mugalu aliifungia Simba bao kwa shuti la kawaida baada ya kupigiwa pasi ya kisigino na Ibrahim Ajibu kisha yeye alimtoka beki mmoja wa Lyon na kupiga shuti.

Goli hilo halikuonyesha kuwavuruga African Lyon kwani waliendelea na utulivu lakini bado Simba walihitaji goli lingine zaidi.

Dakika 54 Simba walipata bao la pili kupitia kwa Charles Ilanfya baada ya kuunganisha kwa kichwa krosi ya Gadiel Michael na mpira ukaenda moja kwa moja wavuni.

Baada ya mchezo huo kocha mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck amesema amefurahishwa na kiwango ambacho wameonyesha wachezaji wake katika mchezo huo.

"Wamecheza vizuri wachezaji wote na ukiangalia kuna wachezaji hawakuwepo hata katika kikosi cha wachezaji 18 kwenye mechi iliyopita lakini leo wamefanya vizuri" amesema Sven.

Sven aliongeza kwa kusema "Mchezo huo ulikuwa ni mchezo wa kirafiki lakini pia kuwapa utimamu wa mwili wachezaji wake ambao hawapati nafasi ya kucheza katika kikosi cha wachezaji 18".

 

PASI ZA VISIGINO

Pasi za visigino zimeonekana kumng'arisha straika wa Simba, Chris Mugalu kwani zimekuwa zikimzalishia mabao.

Mugalu raia wa Congo ameanza kuzoeana taratibu na wenzake tangu asajiliwe na klabu hiyo hivi karibuni.

 

Straika huyo ameonekana kuzitumia vema pasi zote za kisigino anazopewa na wenzake na kufunga mabao maridadi.

Katika mchezo wa leo dhidi ya African Lyon, Mugalu amefunga bao zuri kwa shuti la kawaida dakika ya 47 akimalizia pasi ya kisigino aliyopewa na Ibrahim Ajibu.

Ajibu alimpa pasi hiyo Mugalu nje ya 18 na kisha kumpiga chenga beki mmoja wa African Lyon na kutumbukiza mpira wavuni hivyo kuamsha shangwe uwanjani hapo.

Hiyo ni mara ya pili Mugalu anafunga bao la aina hiyo baada ya Jumapili iliyopita kufunga kama hivyo katika mchezo wa ligi dhidi ya Biashara United.

Katika mchezo huo wa Ligi Mugalu alipokea pasi ya kisigino kutoka kwa Clatous Chama na Kisha kufunga bao la nne katika mchezo ambao Simba ilishinda mabao 4-0 na likiwa bao lake la kwanza msimu huu tangu ajiunge na timu hiyo.

MFUMO

Kocha wa Simba, Seven Vandenbroeck na msaidizi wake Seleman Matola, wamepanga wachezaji wengi ambao  huwa hawapati nafasi  ya kuanza kikosi cha kwanza tangu  Ligi Kuu Bara ianze Septemba 6.

Kocha Sven katika mchezo huu alionekana kubadilika katika mfumo na kuachana na ule wa 4-2-3-1 anaoutumiaga mara kwa mara na ambao huwa anamsimamisha mshambuliaji mmoja na leo kuchezesha mfumo wa 4-4-2 .

Licha ya kwamba alikuwa anawatumia Mugalu na Ilanfya, viungo Ibrahim Ajibu na Miraj Athuman walikuwa wanaongeza nguvu katika eneo la ushambuliaji.

Ukiachana na safu ya mbele, mabeki ambao wamepewa nafasi ya kuanza ni David Kameta 'Duchu', Gadiel Michael, Ibrahim Ame wakisaidiana na Kennedy Juma, huku golini akiwa amekaa Beno Kakolanya.

Imeandikwa na Thomas Ng'itu, Olipa Assa na Oliver Albert.