Kwa Jonas Mkude,Fei Toto anasubiri

Muktasari:

  • Mashabiki wa Yanga wamekuwa wakiamini kuwa, kiungo wao, Fei Toto ama Papy Kabamba Tshishimbi ni wakali kinoma, lakini katika orodha ya Banyai haikuwa na watu hao, huku akisisitiza Mkude na wenzake ni zaidi ya wote waliopo nchini

INAWEZEKANA mashabiki wa Yanga wasiifurahie taarifa hii, ila ndivyo hivyo! Imebainishwa kuwa kiufundi na mautundu, Jonas Mkude ni mkali kuliko Feisal Salum ‘Fei Toto’ anayetamba Jangwani.

Inaeelezwa Mkude ni kati ya viungo bora watatu wanaofunika nchini akiwamo Frank Domayo ‘Chumvi’ wa Azam FC na Hassan Khamis wa Coastal Union.

Haya sio maneno ya Mwanaspoti, ila ni maneno ya Kocha wa Geita Sports, Hassan Banyai ambaye aliwataja viungo hao, akisema wote ni bora ila wametofautiana maujanja. Kisha akampotezea kabisa Fei Toto ambaye ndiye anaonekana mkali kule Yanga.

Banyai, alianza na Hassan aliyewahi kumfundisha akiwa Majimaji ya Songea na kusema kiungo huyo ni kwa sababu tu hachezi kwenye timu zenye majina makubwa kama Simba na Yanga ndio maana anaonekana wa kawaida.

“Khamis ana uwezo wa kuchezesha timu kwenye kushambulia na kukaba, lakini ni kiongozi mchezoni ana uwezo wa kuelekeza wenzake wakapata matokeo mazuri,” alisema Banyai.

Kuhusu Mkude alisema ana akili ya mpira anapopasiwa, anajua aupokee vipi na kuutoa vipi, umiliki na vitu vingi vingine lakini anatakiwa kufanyia kazi tatizo la kucheza pasi za nyuma na ‘square’ pasi.

“Ninaposema pasi za nyuma ni kwamba, kuna wakati badala ya kutoa pasi za mbele yeye anarudisha nyuma na kuchelewesha mashambulizi hilo na mwingine ni Frank Domayo. Domayo kwangu ni ‘fantastiki’ katika kumiliki na kuchezesha,” alieleza Banyai.

Alifafanua na kusema kwa Domayo kinachomsumbua ni majeruhi ya mara kwa mara lakini kama si hivyo, ni mtu hatari kwenye eneo hilo, ila anapokuwa fiti ni noma sana akila sahani moja na Mkude aliyemwagia sifa ni mzoefu zaidi.

Mashabiki wa Yanga wamekuwa wakiamini kuwa, kiungo wao, Fei Toto ama Papy Kabamba Tshishimbi ni wakali kinoma, lakini katika orodha ya Banyai haikuwa na watu hao, huku akisisitiza Mkude na wenzake ni zaidi ya wote waliopo nchini.