Kwa Chelsea muhimu, kwa Liverpool muhimu zaidi

Saturday April 13 2019

 

TEMBEZA bakuli lako la maoni pale Anfield na popote walipo mashabiki wa Liverpool duniani. Waulize, wanataka nini kati ya ubingwa wa England au ule wa Ulaya? Watakujibu wanataka ubingwa wa England. Mara ya mwisho waliuchukua mwaka 1990. Inachosha kurudia.

Kuna timu sita tu ambazo zimewahi kuchukua ubingwa wa Ligi kuu ya England. Manchester United, Blackburn, Arsenal, Chelsea, Manchester City na Leicester City.

Liverpool walichukua wakati huo inaitwa Ligi Daraja la Kwanza.Ubingwa wa Ulaya walichukua mwaka 2005. Sio mbali sana kulinganisha na mwaka 1990. Kiu ya Liverpool ni ubingwa wa England. Huu ndio utarudisha wazimu kwao. Siamini kama Jiji la Liverpool na vitongoji vyake litalala.

Kesho Liverpool wanacheza na Chelsea pale Anfield. Ni mechi muhimu zaidi kwa Liverpool kuliko Chelsea. Kwa nini na Chelsea wapo katika hatari ya kukosa Top Four? Sababu moja kubwa. Kwanza kabisa Chelsea wana mbinu nyingine mbadala ya kuingia michuano ya Ulaya msimu ujao.

Chelsea wanakaribia kutinga hatua ya nusu fainali michuano ya Europa. Mbele yao naona kizingiti cha Arsenal tu lakini vinginevyo wana nafasi kubwa zaidi ya kuchukua ubingwa wa Europa ambao utawapa tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao.

Liverpool hawana mbadala wa kitu chochote kama wakifungwa mechi ya kesho. Sababu ni rahisi tu. Hata wakichukua ubingwa wa Ulaya bado hawawezi kuchukua ubingwa wa England. Kwao ubingwa wa England ni ubingwa wa England tu na hauna mbadala na kitu kingine.

Mechi ya kesho ni fainali kwao. Chelsea watakachopanga ni kutibua tu sherehe za Anfield. Iliwahi kutokea wakati Steven Gerrard alipoteleza na Demba Ba akaenda kufunga. Kama kuna nuksi ambayo wanaomba isitokee ni hii hapa.

Watacheza na Chelsea kwa kumbukumbu ubingwa wa mwisho waliowahi kuukaribia zaidi uliishia katika kiatu cha Gerrard aliyeteleza mbele ya Demba Ba. Zaidi, hii huenda ikawa mechi kubwa ya mwisho kwa Liverpool msimu huu baina ya zile mechi za Top Six.

Sawa mechi ya mwisho watacheza na Wolves ambayo ni ngumu, lakini kwanza ni lazima washinde Anfield kesho. Vinginevyo mechi dhidi ya Wolves inaweza isiwe na umuhimu.

Advertisement