Kuwaona Chama, Fei Toto wakikichafua Simba, Yanga buku saba

Monday February 11 2019

 

By Thobias Sebastian

Dar es Salaam. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limetangaza viingilio vya kuwaona viungo mahiri Clatous Chama wa Simba na Feisal Salum ‘Fei Toto’ katika mchezo wa Watani wa Jadi utakaochezwa Jumamosi hii kuwa ni buku saba (Sh 7,000) na 30,000.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka TFF zinasema kuwa, kiingilio hicho ni cha jukwaa la mzunguko na kwamba katika pambano hilo litakalopigwa saa 11 jioni ni kwamba kila kitu kwa sasa kipo sawa.

Mashabiki wa miamba hiyo watapata nafasi adimu ya kuona ubora wa viungo wao Chama na Fei Toto wakionyesha uwezo wa kutawala katikati ya uwanjani.

Mbali na kiingilio hicho pia, TFF imeweka bayana kiingilio cha juu kitakuwa Sh 30,000 kwa Jukwaa VIP A, huku VIP B na C, watazamaji watalipa Sh 20,000 tu.

Kiungo Mzambia Chama anasifika kwa uwezo wake mkubwa wa kupitisha pasi za mwisho kwa washambuliaji wake Simba, wakati Fei Toto wa Yanga akiwa na sifa ya kukaba pamoja na kupiga mabao ya mashuti akiwa nje ya 18.

Hilo ni pambano la 101 kwa watani hao wajadi ambao walianza kukutana tangu Ligi ilipoasisiwa mwaka 1965 na katika mchezo wao wa mwisho uliokuwa wa 100 timu hizo zilishindwa kufungana.

Advertisement