Kutekwa bosi Simba kwatikisa dunia

Muktasari:

Baadhi ya vyombo vya habari Afrika vilivyorusha habari za Dewji ni pamoja na Daily Nation na The Standard (Kenya), The Monitor (Uganda),  mitandao ya masuala ya biashara kama CBNCAfrica.com, Africaexponent.com, businessinsider.com, Zimbabwesituation.com na businesslive.com.

Kutekwa kwa mfanyabioashara maarufu ambaye ndiye bosi mkuu wa klabu ya Simba, Mohamed Dewji, kumetikisha, si tu Tanzania bali hata anga za kimataifa.
Jarida la Forbes limekuwa likifanya utafiti wake na kumtangaza mara kwa mara Dewji kama mfanyabiashara kijana aliyefanikiwa zaidi, limeandika habari zake.
Forbes lilisema kuwa Dewji anashika nafasi ya 17 kwa utajiri unaofikia Dola 1.5 bilioni.
Vyombo vya habari vya Uingereza, ikiwemo Shirika la Utangazaji, (BBC), Shirika la Habari la Uingereza (Reuters) na baadhi ya magazeti ya; The times, Daily Telegraph, Daily Mail, Irish Times, The Guardian na The Independent yameandika habari za Dewji.
Pia habari za Dewji zimetua Canada ikiwemo gazeti la Ottawacitizen , Voice of America, Sauti ya Ujerumani na Voice of America (VOA).
Kituo cha habari maarufu cha Marekani, CNN kimerusha habari za Dewji pamoja na kituo cha televisheni cha Al Jazeera cha Qatar kimeandika habari za mfanyabiashara huyo.
Dewji inaelezwa ni kati ya wawekezaji wazawa wenye sifa za kutengeneza ajira zaidi ya 20,000 Tanzania na amekuwa akiendesha biashara zake Afrika Mashariki na Kati.
Kupitia Kampuni yake ya METL Group, ameweza kumiliki viwanda zaidi ya 35 katika masuala mbalimbali ikiwemo; kilimo, uzalishaji mali, masuala ya nishati ya gesi na petroli, huduma za fedha, simu za mkononi, mashamba na maeneo ya makazi, usafirishaji, na usambazaji.