Kuna muvi la mapenzi ya kibabe pale WCB

Sunday May 12 2019

 

By LUQMAN MALOTO

KARIBU saana kwenye hili muvi. Linaitwa Mapenzi ya Kibabe. Ukipenda liite Mapenzi ya Kindava. Linachezwa na majanki wa ngome kubwa ya muziki Bongo na Afrika, Wasafi Classic Baby (WCB).
Kukutafsiria muvi hili ni mimi msimuliaji wako, Luqman Maloto wa Mwanaspoti, ikikupendeza niite Lufufu wa Mwanaspoti. Katika muvi hili, Mkurugenzi wa WCB, Diamond Platnumz, amecheza kama bosi asiye na siri. Mnokomnoko yaani. Siri za watu wake anaziingiza kwenye nyimbo zake.
Ndani ya muvi utakutakana na staa mkali sana wa Bongo Fleva, Harmonize na sweetbebi wake wa Kizungu, Sarah. Penzi lao likaingiliwa ikawa shughuli. Mtu mbabe, mbavu nene, Mwarabu Fighter amecheza kama jamaa fulani mnyonge, lakini akadondokewa na zali la kupendwa na mke wa bosi wake. Mwanamke Mzungu. Yakamkuta makubwa.
Mrembo Jacqueline Wolper amecheza sehemu ndogo ya mwanamke aliyetendwa. Aliumia mno alipoachwa na mwanaume wake kisa amepata mwanamke wa Kizungu. Baadaye Wolper anaonekana akila raha kushangilia taarifa za mwanaume aliyemwacha, kusalitiwa na mwanamke wa Kizungu.
Dansa namba moja wa WCB, Mose Iyobo yupo ndani. Amecheza pati yake na bebi mama wake, Aunty Ezekiel. Penzi lao likazingirwa na gogoro zito. Aunty akaruka na mwanaume mwingine. Shoo nyingi za mitandaoni, Aunty akiwa chumbani na mwanaume mpya.
Location ya muvi hii kwa sehemu kubwa imechezwa Instagram. Huko insta kuna bi'dada ana umbea wote mjini. Hata wewe hapo, anaweza kukwambia michepuko yako yote na ya mpenzi wako. Ladies and gentlemen, namtambulisha Mange Kimambi kama staa mwingine aliyecheza muvi hii.

MUVI LIANZE SASA!
Inaanza hivi; Harmonize akiwa bado hajatoboa kihivyo. Yaani bado mwenye tongotongo za 'uandagraundi', anaingia kwenye penzi na mrembo supastaa mkubwa, Wolper. Ooh, penzi linakolea. Janki anaamua kumuimbia wimbo Wolper, unaitwa ‘Niambie’. Wakarekodi na video Bondeni. Ndani ya wimbo Harmonize anamlilia Wolper asimtende.
Mara penzi linageuka shubiri. Wolper machozi mengi yanachirizika mashavuni mpaka yanatibua make-up na kumfanya aonekane rangi mbili. Kumbe analizwa na taarifa za Harmonize kupata mwanamke wa Kizungu. Ana mapene sana. Anaitwa Sarah!
Pamoja na vilio na jitihada za Wolper za kila aina, anashindwa kumrejesha Harmonize kwenye himaya yake. Harmonize anaamua kuutuliza kwa Sarah. Janki anazidi kufanikiwa kimuziki. Maisha mpeto na Mzungu wake. Wanafanikisha ujenzi wa mjengo wa ghorofa. Hatari sana!
Mwarabu Fighter ni bodyguard wa Diamond Platnumz. Yule bosi mbeambea wa WCB, asiyetunza siri za wafanyakazi wa chini yake. Harmonize ni msanii wa WCB. Hivyo, Diamond ni bosi wa wote wawili, Harmonize na Mwarabu.
Mwaka jana Mei, bi'dada mwenye umiliki wa umbea mwingi mjini. Tajiri wa umbea, Mange Kimambi, aliliamsha dude insta. Akafichua siri kwamba Mwarabu Fighter alitimuliwa kazi WCB. Akasema kosa la Mwarabu ni kumdandia Sarah, yule Mzungu wa Harmonize.
Harmonize akapost insta, akasema bora hata angesemwa mwingine, kwamba Mwarabu wa watu hata kuongea hajui. Mwarabu naye akakanusha kutoka na Sarah wa Harmonize. Kimsingi, kila upande ukakanusha. Mange akasisitiza ni kweli Mwarabu alifanya kweli na Harmonize. Kwamba Sarah mwenyewe ndiye alimtamani mbavu nene. Alisuuzika na ile miraba minne ya Mwarabu.
Hata hivyo, ikathibitika kweli Mwarabu alitemeshwa ajira WCB. Upande wa uongozi wa WCB haukutaka kuzungumzia chochote. Mwarabu alisema aliacha kazi mwenyewe baada ya kuona hapewi mshahara miezi mitatu mfululizo, yaani Februari mpaka Mei. Hata kazi alikuwa hapangiwi tena.
Kipande kingine anaonekana Wolper akishangilia ubuyu kutoka kwa Mange. Wolper hujiita Wolper Gambe, yaani Wolper Kilaji. Wolper Ulabu. Wolper Mitungi. Ni mzuri sana kwa kupombeka. Katika ushangiliaji wake, Wolper anapiga matingasi kufurahia habari za Sarah kumsaliti Harmonize kwa Mwarabu.
"Si alijifanya ananiacha kwa sababu ya Mzungu wake. Ona sasa, Mzungu naye kamfanyia utafiti wa kitandani Mwarabu. Ndo akomage huko. Unaniacha mimi unaenda kwa Mzungu. Mwarabu hoyee! Mwarabu utabaki kileleni. Mwarabu alamba lolo," Wolper alisherehekea kinomanoma!

MWAKA UKAPITA
Habari za Mwarabu na Sarah hazisikiki tena. Watu walishasahau. Si unajua Bongo umbea ni sogea tukae? Ukitoka huu unakuja mwingine. Wakati mwingine miubuyu inapandiana tu mpaka mlaji anachanganyikiwa ale upi aache upi. Ni kama sasa, antena zinanasa masafa ya kwa Askofu Josephat Gwajima. Sitaki shobo. Tuliza mshono! Tuendelee na muvi letu la Mapenzi ya Kindava WCB.
Mwaka umepita, Mwarabu na Sarah siyo topic tena! Ghafla bosi mnoko, Diamond, kaachia wimbo unaitwa "Inama". Akaimba: "Mapenzi yalisababisha Harmonize amfukuzishe Mwarabu."
Mange akarudi hewani. Akakinukisha insta: "Mmeona sasa? Niliwaambia kisa cha Mwarabu kutimuliwa WCB ni kumfanyia utafiti wa kitandani Sarah wa Harmonize mkabisha? Diamond ameimba sasa kuwa Harmonize ndiye alimfukuzisha Mwarabu." Watu wakabaki ooh!
Harmonize naye akaamua kumjibu Diamond insta, akasema: "Hii ni kunivunjia heshima kuutangazia umma kuwa mke wangu alifanyiwa kitu kamili na Mwarabu." Mpaka hapo Diamond akawa kathibitika ni bosi asiye na koromeo. Hana kifua. Siri za watu wake anaziingiza kwenye wimbo.
Kuna mwana akaniambia: "Diamond mambo yake mwenyewe huwa hana siri. Mikasa yote ya kimapenzi na wanawake zake mpaka na mama wa watoto zake, inajulikana kwa kila mtu, itakuwa siri za mapenzi ya kina Harmonize na Mwarabu?" Nikatikisa kichwa kuonesha nimeelewa.

SCENE NYINGINE
Ni yuleyule Diamond, bosi asiye na siri, hapa anatokeza kwa dansa wake, Mose Iyobo. Wanarekodi kipande cha video kuutangaza wimbo, "Inama". Ni kipindi ambacho imeshavuja kwamba Iyobo amewekwa kushoto na mama mtoto wake, Aunty Ezekiel.
Tayari Aunty ameshamtambulisha mshika moyo mpya. Shughuli pevu ipo insta. Mipicha ya chumbani na huyo brand new mwenye moyo wa Aunty. Diamond akaoni ni opotyuniti ya kuupa busta wimbo wake.
Mose Iyobo ameshika tama, Diamond anamuimbia: "Penzi kwa wanangu limeleta vita. Siku hizi simuoni. Naishia tu kuona insta. Asiyekupenda acha naye. Anayekupenda pendana naye." Iyobo na Diamond wanasimama kucheza, wimbo unaagiza kuacha stess, kucheza na kufurahi. Wakainama kweli kupindisha mgongo.
Aunty akaja mwenyewe. Akapost wimbo wa Diamond. Ule wimbo huanza na maneno: "Hukudekuza kama mtoto, furaha unafurahia." Aunty akaandika: "Kukudekeza kama mtoto furaha unafurahia. Mkasahau mkaona hawa wamama mafala. Hapa unaachwa na sebene tunacheza na new baby kama kawa. Endeleeni kupeana moyo."
Yaani Aunty aliielewa mistari ya wimbo kuwa analengwa yeye na ile sehemu Diamond na Iyobo wanacheza sebene kuonesha wanaweka kando stress za mapenzi ni kupeana moyo. Akawajibu naye sebene anacheza na mpenzi wake mpya.
Kule Harmonize, Sarah na Mwarabu, huku Iyobo na Aunty, katikati bosi kubwa Diamond, yaani ni muvi la mapenzi ya kindava WCB.

Advertisement