Kuna mtu atapasuka Kirumba

Muktasari:

Nahodha Msaidizi wa Yanga, Juma Abdul alisema wanaingia uwanjani kwa umakini sana kuhakikisha wanashinda mchezo huo ili kuendelea kuweka pengo dhidi ya Simba na Azam.

MWANZA.VINARA wa Ligi Kuu Bara, Yanga wanafahamu hakuna namna nyingine ya kuwakimbia Azam FC na Simba kwenye mbio za ubingwa ila kushinda mechi zao na jioni la leo Jumatatu watakuwa Uwanja wa CCM Kirumba kusaka alama tatu muhimu dhidi ya African Lyon, huku pande zote zikichimba mkwara mzito.

Yanga imetamba kama Lyon inapiga hesabu za kujinusuru kushuka daraja kupitia mgongo wao, basi waendelee kujidanganya, kwani ukweli ni lazima wapasuke, huku wapinzani wao wakicheka kwa dharau na kusema ‘thubutu yenu’.

Yanga inavaana na Lyon katika mchezo wa kwanza ikiutumia Uwanjwa wa Kirumba kama wa nyumbani baada ya Uwanja wa Taifa kufungwa, huku ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya 1-1 na Ndanda FC katika mchezo uliopita.

Nahodha Msaidizi wa Yanga, Juma Abdul alisema wanaingia uwanjani kwa umakini sana kuhakikisha wanashinda mchezo huo ili kuendelea kuweka pengo dhidi ya Simba na Azam.

Alisema kisaikolojia na morali kwa wachezaji wote iko vizuri, hivyo matarajio yao ni kushinda na kuwataka wenzake kwa kila mmoja kujituma.