Kuna kocha anasema Paul Pogba hakabiki eti

Muktasari:

Kocha Puel hakuna jambo jingine zaidi ya kumsifu tu kiungo huyo wa Manchester United, ambaye asisti yake ndiyo iliyoamua matokeo ya mechi hiyo wakati wababe hao waliposhinda 1-0 uwanjani King Power, shukrani kwa bao la Marcus Rashford.

LEICESTER, ENGLAND.KOCHA wa Leicester City, Claude Puel amesema kiungo Paul Pogba amemshindwa kabisa kwa sababu huwezi kumdhibiti kwa kumwekea mchezaji mmoja.

Kocha Puel hakuna jambo jingine zaidi ya kumsifu tu kiungo huyo wa Manchester United, ambaye asisti yake ndiyo iliyoamua matokeo ya mechi hiyo wakati wababe hao waliposhinda 1-0 uwanjani King Power, shukrani kwa bao la Marcus Rashford.

Katika mechi hiyo iliyofanyika Jumapili iliyopita, Puel alimpa mchezaji mmoja majukumu ya kumkaba Pogba, lakini mambo yalikuwa mazito na mtu wake hakufua kabisa dafu katika kufanya kile alichostahili kukifanya ndani ya uwanja.

“Pogba? Huwezi kumpangia mtu mmoja amdhibiti. Ana nguvu, anakwenda mbele kwa haraka sana,” alisema kocha huyo.

“Tulishindwa kabisa kumdhibiti. Zile nguvu zake vigumu kabisa kumtuliza. Ana akili pia ya mpira, kwani anapokwenda mbele anakuwa hatari sana. Ana macho ya ziada kwenye mchezo.

“Akigusa mpira mara moja tu au mbili, basi baada ya hapo kile anachofanya kwenye mpira huo ni ubunifu mkubwa.

“Anaona kwa haraka sana na huo ni ufundi mkubwa. Lakini, kingine kuna wachezaji wengi wachapa kazi wamekuwa wakicheza kumzunguka yeye. Hiyo ndiyo Manchester United tuliyomenyana nayo, ndio Man United ya sasa.”