Kuna Mbongo alitesa Kombe la Dunia kule Afrika Kusini

Muktasari:

  • Mbongo huyo ambaye kiasili ni mtu wa Tanga, aliweka rekodi hiyo kwenye mchezo dhidi ya Peru uliomalizika kwa Denmark kuitandika timu hiyo bao 1-0.

YALIYOPITA si ndwele. Miaka minane iliyopita kwenye ardhi ya mtu, ambaye alipewa heshima kubwa enzi za uhai wake kama Mkombozi wa Bara la Afrika, Nelson Mandela kipindi cha Kombe la Dunia, Tanzania ilikuwa na mwakilishi wake huko.

Usishtuke maana kumbukumbu zako zinaweza kukurejesha mbali kwa kuwaza kwa sababu hata Afcon tumewahi kushiriki mara moja iwaje tulikuwa na mwakilishi Kombe la Dunia wakati hatukuwa miongoni mwa mataifa 32 yaliyokuwa na tiketi.

Uwakilishi wa Tanzania ulikuwa kama ule wa msimu huu wa Kombe la Dunia pale Russia, kwa kuwa na nyota mwenye asili ya taifa letu, bila shaka mpaka hapa taratibu tumeanza kwenda sawa.

Kabla ya kuanza kwa michuano ya Kombe la Dunia Russia kwenye kikosi cha cha Denmark kilichokuwa chini ya kocha wao, Åge Hareide aliitwa Yussuf Yurary Poulsen wa RB Leipzig, ambaye ana asili ya Tanzania pamoja na mshambuliaji mwingine hatari, Nicklas Bendtner.

Kupata majeraha kwa Bendtner aliyewahi kuichezea Arsenal ni kama kulibariki safari ya Poulsen, ambaye aliweka rekodi Juni 16, 2018 kwenye Uwanja wa Mordovia uliopo kwenye Mji wa Saransk, Russia ya kuwa nyota wa kwanza mwenye asili ya Tanzania kucheza na kufunga bao kwenye michuano hiyo.

Mbongo huyo ambaye kiasili ni mtu wa Tanga, aliweka rekodi hiyo kwenye mchezo dhidi ya Peru uliomalizika kwa Denmark kuitandika timu hiyo bao 1-0.

Lakini kumbe mzizi wa Wabongo kulichezea taifa hilo, ulianza kuota tangu 2010 kwenye kikosi chake wakati wa kombe hilo la dunia ambalo lilifanyika kwa mara ya kwanza kwenye ardhi ya Afrika, walikuwa na Patrick Mtiliga. Ndio! Kikosi kile cha Denmark ambacho kilikuwa na chipukizi kama, Christian Eriksen ambaye alikuwa na miaka 18, kilikuwa na Patrick ambaye kwa sasa ametundika daluga zake.

Patrick aliyezaliwa Januari 28, 1981 kwenye Mji wa Copenhagen, Denmark ni mtoto ambaye baba yake, Mzee Patrick ni Mtanzania. Alianza kucheza soka kwenye klabu ya vijana ya Boldklubben katika mji aliozaliwa.

Kufanya kwake vizuri kwenye kikosi hicho, kulimfanya umri uliposogea wa kuanza kucheza soka la kulipwa kusajiliwa na Feyenoord Rotterdam, iliyokuwa Ligi Kuu Uholanzi ambayo ni maarufu kama Eredivisie, mwaka 1999.

Akiwa beki wa kushoto, Patrick alitolewa kwa mkopo kwenda Excelsior Rotterdam iliyokuwa madaraja ya chini kwa lengo la kwenda kupata uzoefu.

Patrick aliingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza cha Excelsior ambayo aliichezea kwa mafanikio makubwa ikiwemo kuchangia kupanda daraja msimu wa 2001–02.

Lakini kibaya kwao walijikuta msimu uliofuta kwenye Eredivisie wakirejea tena Ligi Daraja la Kwanza Uholanzi.

Baada ya kuonekana amekomaa, Patrick alirejeshwa na klabu yake ya Feyenoord na mara baada ya kurejea alipata nafasi ya kucheza michezo 11 ya Eredivisie hadi pale ambapo alipopata majeraha, Januari 2005 yaliyomweka nje hadi 2006.

Agosti 2006, Mbongo Patrick alijiunga na wapinzani wa Feyenoord, NAC Breda kwa kusaini mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuuongeza muda wowote.

Kufanya kwake vizuri kuliishawishi timu hiyo kumuongezea mkataba wa miaka miwili.

Neema ili mshukia Patrick ambaye alipata dili la kujiunga na Malaga CF inayoshiriki Ligi Kuu Hispania, 2009 ambako Januari 24 mwaka uliofuata alimkaba Cristiano Ronaldo kwenye La Liga pale timu yake ilipokutana na Real Madrid.

Katika mchezo huo, Ronaldo alionyeshwa kadi nyekundu kwa kuchezea vibaya Mbongo huyo, ambaye baadaye akaitwa kwenye kikosi cha Denmark ambacho kiliishia hatua ya makundi kwenye Kombe la Dunia Afrika kule Kusini mwaka 2010.

Bahati mbaya kwake ni kuwa alishindwa kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza mwenye asili ya Tanzania kucheza Kombe la Dunia kutokana na kutopata nafasi ya kucheza mbele ya Simon Poulsen aliyekuwa akiichezea Sampdoria ya Italia.

Baada ya kushindwa kuweka rekodi hiyo mwaka uliofuata, Agosti 2011, aliamua kurejea Denmark kwa kujiunga na Nordsjælland kwa mkataba wa miaka miwili.

Ulipomalizika tu mkataba wake alitangaza kutundika daluga hakika yaliyopita si ndwele tuendelee kusubiri yajayo baada ya miaka mingine minne ili yatufurahishe.