Kumuyange watangaza vita baada ya kichapo

Muktasari:

  • Kumuyange ilichezea kichapo cha mabao 3-2 kutoka kwa Milambo FC sasa kocha wake Shedan Magege ameapa kufa na Area C katika mchezo utakaopigwa wilayani Ngara jumamosi ya wiki hii.


JUZI Jumapili Kumuyange FC iliipunguzwa kasi kwa kudundwa mabao 3-2 dhidi ya Milambo FC katika mchezo wa Ligi Daraja la Pili lakini Kocha wa timu hiyo, Shedan Bagege amekubali kichapo hicho na sasa hasira zao watazimalizia Area C.

Kumuyange ilianza kwa kasi michuano hiyo ya Daraja la Pili na kujikita nafasi ya pili lakini kichapo cha juzi mkoani Tabora kiliwashusha hadi nafasi ya tatu kwa pointi sita baada ya mechi nne.

Bagege alisema sasa wanarudi wilayani Ngara ambapo wanajipanga mchezo wao wa Jumamosi dhidi ya Area C ili kupata alama tatu.

Aliongeza kuwa mchezo huo hautakuwa rahisi kutokana na wapinzani wao kuhitaji ushindi baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo hivyo wanahitaji pointi tatu ili kujiweka nafasi nzuri.

“Tumepoteza mchezo dhidi ya Milambo kwa matakwa ya Mwamuzi na si kwa kiwango kidogo cha wachezaji wangu, hayo yamepita na sasa tunaenda kuhakikisha mechi ijayo tunashinda,” alisema Kocha huyo.

Kocha wa Area C, Mathias Wandiba alisema kamwe hawatokubali kuondoka Kanda ya Ziwa kwa kuchezea vichapo vitatu mfululizo hivyo wanajipanga kuhakikisha wanapata ushindi dhidi ya Kumuyange.

“Tumejipanga, hatuwezi tena kupoteza mchezo mwingine tutapambana kuhakikisha tunapata ushindi dhidi ya Kumuyange,” alisema Wandiba.