Kumkaba Kagere, Tariq ujipange

BEKI wa Ruvu Shooting, Rajab Zahir amesema kuwabaka washambuliaji Tariq Seif wa Yanga na Meddie Kagere wa Simba inahitaji akili nyingi kwani wachezaji hao ni wajanja wajanja.
Zahir ameweka wazi kauli hiyo kwamba nyota hao mara nyingi huwapa kazi ngumu mabeki wengi kuwadhibiti.
Zahir amesema inahitaji kutumia nguvu na akili muda wote pamoja na umakini kuongezeka unapocheza na washambuliaji hao zaidi ya hapo utajikuta wametupia kambani na kukutia lawama.
Amesema kwa upande wa Kagere ni mshambuliaji ambaye muda wote unatakiwa kucheza naye kwa uangalifu pia kuhakikisha hapigi mipira ya vichwa na hapati nafasi ya kucheza.
“Kagere ni msumbufu sana lakini ili angalau uweze kumthibiti inatakiwa ucheze naye kazi kazi na uhakikishe muda wote wa mchezo unakuwa naye makini hasa kwenye mipira ya vichwa ambayo kwake huwa ni mzuri sana,”amesema Zahir.
Beki huyo amesema kwa upande wa Seif naye anahitaji maarifa zaidi kwani ni straika mjanja mjanja na muda wote huwa hatulii sehemu mmoja ndani ya uwanja na anahitaji umakini ili kuhakikisha hapati nafasi ya kufunga.
Amesema mara nyingi anapocheza na mshambuliaji huyo anakuwa makini naye hasa kwenye mipira ya vichwa na pia kumzuia asipige mashuti ambayo mara nyingi anafunga mabao ya aina hiyo.
“Angalia mabao anayofunga Seif unaona kabisa mabeki walimsahau na ndio mchezo wake hivyo unahitaji sana kuwa makini kumkaba mara nyingi unajikuta unapata lawama kwani ukizubaa tu kakufunga ni mshambuliaji mjanja mjanja ana mambo mengi zaidi ya kufunga,” amesema