Kumekucha sasa Rais Magufuli aongeza mzuka upya

Friday May 22 2020

 

By MASOUD MASASI MWANZA

BAADA ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli kutangaza michezo mbalimbali iliyosimama irejee kuanzia Juni Mosi, makocha, viongozi na wachezaji wa Ligi zote wamepiga shangwe la maana.

Mwenyekiti wa Yanga, Mshindo Msolla aliiambia Mwanaspoti jana kwamba uamuzi huo ni wa kupongezwa sana kwavile utaleta usawa kwenye michezo na kumfanya kila mtu avune kile alichopanda bila kubebwa na uamuzi wa mezani.

“Ni uamuzi mzuri sana ambao utafanya kila kitu kiamuliwe uwanjani kulingana na uwezo na kwenye michezo yote, lakini lazima kila mmoja wetu aendelee kujikinga na kufuata maelekezo ya wataalam wa afya,” alisema Msolla na kusisitiza kwamba wao wanajipanga kurejea kwenye programu zao.

Kocha wa Yanga, Luc Eymael amesisitiza kwamba wakipata tizi la wiki tatu tu linatosha kuwaweka sawa tayari kwa ushindani na kutoa utamu zaidi kwenye ligi hiyo huku akili zao zikiwa zaidi kubeba taji la FA.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa amesisitiza kwamba wao wako tayari kurudi uwanjani hata katika kipindi cha mapumziko mafupi walikuwa wanaendelea na program mbalimbali za kiufundi.

Katibu wa Mbao FC, Johnson James alisema wamepata nguvu upya baada ya Rais kuruhusu michezo kuendelea na sasa wanakutana kama viongozi kuona wanajipangaje kuhakikisha wanamaliza mechi nne za Daraja la Kwanza zilizobakia.

Advertisement

Alisema mechi hizo nne ni muhimu kwao kupata ushindi kwani mpaka sasa wako nafasi ya saba wakiwa na pointi 22 hivyo wakifanya vibaya basi msimu ujao wanaweza kushuka daraja.

Kocha wa Gwambina FC, Athumani Bilali ‘Bilo’ alisema aliposikia kauli hiyo ya Rais Magufuli alilipuka kwa furaha na sasa wanasubiri kauli ya viongozi wao lini watarejea kambini kujiandaa na Ligi Daraja la Kwanza ambapo wako wanaongoza kundi B wakiwa na alama 40.

“Tutakuwa makini pia maana Rais wetu amesema huu ugonjwa bado upo hivyo tutafanya mazoezi huku tukiwa makini pia kujilinda na maambukizi ya huu ugonjwa,” alisema Bilo.

Straika wa Biashara United, Victor Hangaya alisema baada ya kauli hiyo mzuka umerejea tena kwani alishakata tamaa kama ligi itaendelea msimu huu.

“Tunasubiri simu za viongozi wetu ili kurejea kambini,” alisema Hangaya huku Kipa wa Alliance FC, John Mwanda akisema kwake ilikuwa kama sherehe ambapo kikubwa sasa ni kujipanga wao kama wachezaji kuhakikisha wanafanya vizuri katika mechi tisa walizobakiza.

“Unajua kwangu nilishakata tamaa maana niliona msimu huu ndio basi tena ligi haitaendelea lakini Rais ametuangalia sisi vijana wake ambao soka ndio ajira yetu kubwa,” alisema Mwanda.

Straika wa Mbao FC, Ndaki Robert alisema; “Uzuri sisi kama wachezaji tulikuwa tunawasiliana wenyewe kwa wenyewe na tulikubaliana tufanye mazoezi ya nguvu katika kipindi hiki ambacho ligi imesimama hivyo tukirejea tutakuwa fiti.”

Advertisement