Kumekucha, silaha za Zahera zatua Dar

Muktasari:

  • Wengine wawili ni mshambuliaji kutoka Nigeria, Shehu Magaji Bulama na kiungo Allex Komenan kutokea Ivory Coast.

SIKU chache baada ya Kocha wa Yanga, Mkongomani Mwinyi Zahera kutangaza kusajili nyota sita wa kigeni na wawili wa ndani kabla hajatimikia Congo, uongozi wa klabu hiyo umeshusha nyota wanne wa kigeni kwa ajili ya kumalizana nao.

Kocha Zahera katika kuhakikisha hafanyi utani kuisuka Yanga na kuipokonya taji la Ligi Kuu Bara Simba msimu ujao na kufanya vizuri katika Kombe la Shirikisho (FA), ili kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa.

Vifaa hivyo vinne kutoka vilitua mazoezini katika Uwanja wa Police College Kurasini jana Ijumaa wakati Yanga ikijiandaa kucheza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC, Aprili 28.

Mwanaspoti liliwashuhudia kiungo kutoka Nigeria, Victor Patrick Akpan mwenye umri wa miaka 20 anayechezea Timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 23.

Kwa sasa nyota huyo anakipiga katika kikosi cha kwanza cha JKU ya Zanzibar.

Mwingine ni beki wa kati, Mohamed Ali Camara akitokea Guinea ambako anafanansiha uchezaji wake na beki wa kati wa Barcelona, Gerard Pique kwa mujibu ya baadhi ya mtandao ya nchi hiyo.

Camara amezaliwa Agosti 28, 1997, umri wake miaka 21, Kerouane, Guinea, alianza kuitumikia klabu ya Young Boys , mwaka 2016–17, alijiunga na Horoya kabla ya kumtoa kwa mkopo katika Timu ya Hafia.

Zahera mara kwa mara amekuwa akihusishwa na mmoja kati ya mabeki wa kati kutoka Guinea na huenda akawa Camara ambaye mbali ya kucheza katika eneo hilo la ulinzi amekuwa akifunga mabao.

Msimu wa 2017/18 alitolewa kwa mkopo kwenda Hapoel Ra’anana na alikocheza mechi 29, na kufunga mabao matatu.

Mwaka 2018, alikuwa katika kikosi cha Young Boys na amecheza michezo mitano na kufunga bao moja.

Katika Timu ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 20, amecheza michezo minane na kufunga bao moja lakini katika timu ya taifa ya wakubwa amecheza mchezo mmoja.

Yanga inaweza kumnasa Camara kutokana mchezaji huyo kumilikiwa na Horoya ya Guinea ambayo imeshia hatua ya robo fainali msimu huu Ligi ya Mabingwa Afrika lakini klabu hiyo ina ukaribu na Yanga kwani imemsajili mshambuliaji wa timu hiyo, Heritier Makambo ambaye mwishoni mwa msimu atajiunga na klabu hiyo.

Wengine wawili ni mshambuliaji kutoka Nigeria, Shehu Magaji Bulama na kiungo Allex Komenan kutokea Ivory Coast.

MSIKIE ZAHERA

Kocha Zahera alisema mara baada ya mchezo dhidi ya Azam atatangaza majina ya nyota wake wapya na pia kutaja majina ya watakaochwa na wale watakaoendelea na kikosi hicho.

“Kabla ya kuondoka hapa nchini kwenda nyumbani Congo likizo nitakuwa nimeshakamilisha usajili wa wachezaji nitakaowahitaji lakini pia nitakuwa nishatambua ambao mikataba yao inamalizika na nitataka uongozi uwaongezee ili niwe nao msimu ujao,” alisema Zahera.

MAKAMU MWENYEKITI AFUNGUKA

Akizungumza na Mwanaspoti, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela alikiri kuwepo kwa wachezaji hao na kusema mazungumzo bado yanaendelea na muda ukifika kila kitu kitawekwa wazi.

Mwakalebela alisema wamewapokea nyota hao jana Ijumaa wakiwa na hadi sasa bado hawajamalizana nao lakini wamewaruhusu kufanya mazoezi wakiwa chini ya Kocha Zahera.

Mwakalebela alisema kama kocha ataridhishwa na viwango vyao hawatakuwa na muda wa kupoteza zaidi ya kuwasanisha mkataba.

Alisema kwa kuwa dirisha la usajili lipo jirani wameona waanze mipango ya usajili wakiwa bado hawajaachana na kocha ambaye ataenda kukiongoza kikosi cha Timu ya Taifa ya Congo katika Mashindano ya AFCON akiwa kocha msaidizi.

“Nyota hao hawajapatiwa mikataba hadi pale kocha atakapotoa uamuzi na wameletwa kutokana na mahitaji ya mwalimu katika kikosi huku akiweka wazi kuwa endapo watakidhi mahitaji ya mwalimu watasajiliwa kwa gharama yoyote,” alisema Mwakalebela.

Ingawa Kocha Zahera amekuwa msiri kuwataja wachezaji atakaowatema katika kikosi chake, lakini nusanusa za Mwanaspoti zimebaini straika Amissi Tambwe na kiungo, Thabani Kamusoko siku zao Jangwani zinahesabika.

MRATIBU NAE

Katika hatua nyingine, Mratibu wa Yanga, Saleh Hafidh alisema wachezaji wote wa Yanga waliokuwa wanaumwa na kuukosa mchezo dhidi ya Mbeya City wamesharejea mazoezii kasoro Gadiel Michael.

MSIKIE FEI TOTO

Kiungo fundi wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amekiri kumfahamu kiungo aliyetokea visiwani Zanzibar kuwa ni mchezaji mzuri na ana umri ambao unaweza kuisaidia timu kwa miaka ya hivi karibuni. Fei Toto alijiunga na Yanga akitokea JKU ya Zanzibar klabu ambayo anachezea Mnigeria huyo ambaye jana alifanya mazoezi na Yanga.