Kumbuka jezi za mastaa hawa zimestaafishwa

Muktasari:

Klabu mbalimbali barani Ulaya zimekuwa na utamaduni wa kuacha kutumia jezi za baadhi ya nyota wao waliocheza kwa mafanikio katika klabu zao

LONDON, ENGLAND. HESHIMA ni kitu muhimu. Kuna mastaa waliofanya mambo makubwa katika soka ambayo yamesababisha kustaafu kwao, au kupoteza kwao maisha kumepelekea jezi zao zistaafishwe kama heshima maalumu kwao. Hawa ni baadhi ya mastaa ambao jezi zao hazitumiki tena klabuni.


 Marc-Vivien Foe (Man City #23)
Kiungo mahiri wa zamani wa kimataifa wa Cameroon ambaye alikuwa kipenzi cha mashabiki wengi wa soka ulimwenguni kote. Bahati mbaya alipoteza maisha yake katika pambano la Cameroon dhidi ya Colombia mwaka 2003 katika michuano ya Mabara nchini Ufaransa. Hiyo ilikuwa mechi yake ya 64 kwa timu ya taifa ya Cameroon. Kabla ya hapo alikaribia kujiunga na Manchester United mwaka 1999 lakini akavunjika mguu. Baada ya kifo chake, jezi namba 23 aliyokuwa anavaa Manchester City ilistaafishwa lakini pia klabu yake nyingine aliyopitia, Lens waliistafisha jezi namba 17.

 Gianfranco Zola (Chelsea #25)
Licha ya kwamba Chelsea hawakutangaza rasmi kuistaafisha jezi namba 25, lakini hakuna mchezaji mwingine yeyote aliyekuwa amepewa kuvaa hiyo jezi kwenye kikosi hicho kwa kipindi cha miaka 15 tangu Zola alipoondoka. Beki John Terry aliripotiwa alichukua jezi yenye namba 26 ili tu aweze kuwa karibuni na Zola kwenye makabati yao huko kwenye vyumba vya kubadilishia. Kuna uwezekano mkubwa hata hiyo namba ya Terry nayo ikastaafishwa huko Stamford Bridge na kufanya tukio la wawili hao waliotaka kuwa pamoja jezi zao kutotumika tena kwenye kikosi hicho cha The Blues kwa heshima.

Paolo Maldini (Milan #3)
Huko kwenye kikosi cha AC Milan kwa sasa huwezi kuona tena jezi yenye namba 3 ikivaliwa na mchezaji yeyote kwenye timu hiyo kwa sababu imestaafisha. Ilikuwa ikivalkiwa nna Paolo Maldini, gwiji wa Kitaliano, aliyeichezea timu hiyo mechi 902 kwa kipindi cha misimu 25. Maldini aliyefahamika kama ‘Il Capitano’ anashikilia tekodi ya kucheza mechi nyingi za Serie A kwa klabu hiyo, akicheza mara 647 na kubeba mataji saba. Alistaafu mwaka 2009 akiwa na umri wa miaka 41 na jezi yake ikastaafishwa pia kwa heshima.

Javier Zanetti (Inter #4)
Ac Milan na wapinzani wao Inter Milan wote wanatumia Uwanja wa San Siro kwa mechi zao za nyumbani. Wakati mashabiki wa Milan wakikosa fursa ya kuona jezi yenye tatu mgongoni kwa mchezaji mwingine katika kikosi chao kwa sasa, mahasimu wao Inter nao hawatakuwa na nafasi ya kuona jezi yenye namba nne mgongoni ikitumika. Jezi hiyo imestaafishwa kwa heshima ya Muargentina, Javier Zanetti, ambaye alikuwa mtumishi mzuri wa timu hiyo ya Italia. Inter wameamua kuipumzisha jezi namba nne kwa heshima ya Zanetti.

Diego Maradona (Napoli #10)
Kuwaongoza Napoli kwenye ubingwa wa mataji mawili ya Serie A yalitosha kabisa kwa Maradona kuwa shujaa huko Naples. Maradona alikuwa moto pia kwenye Coppa Italia, Kombe la UEFA na Italian Super Cup akiwafanya Napoli kutamba na ndiyo maana haikuwa shida kwa klabu hiyo kuamua kuistaafisha jezi namba 10 kwa heshima ya gwiji huyo wa soka wa Argentina. Hakuna mchezaji mwingine aliyefanya mambo makubwa zaidi kwenye kikosi cha Napoli kuliko Maradona na ndiyo heshima yake inabaki kuwa juu kwenye kikosi hicho.

Raul (Schalke #7)
Wakati Cristiano Ronaldo anatua Real Madrid alikuta jezi namba 7 ilikuwa ikivaliwa na Raul, hivyo akalazimika kuvaa jezi namba 9 kwa muda hadi hapo fowadi huyo wa Kihispaniola alipotimkia zake Ujerumani kujiunga na FC Schalke 04. Raul alipotua Schalke, alikabidhiwa jezi namba 7, lakini kwa huduma yake ya miaka miwili tu aliyocheza kwenye timu hiyo, Schalke waliamua kuistaafisha jezi hiyo kwa muda kutokana na heshima ya kuona mchezaji kama Raul anakwenda kucheza kwenye timu yao. Hata hivyo baada ya mwaka mmoja kupita, Schalke waliirudisha jezi hiyo wakimpa kinda wao matata, Max Meyer.

Bobby Moore (West Ham #6)
Bobby Moore alikuwa bonge la staa kwenye soka na alidumu kwenye kikosi cha West Ham United kwa miaka 16, katika kipindi ambacho aliisaidia pia England kubeba ubingwa wa Kombe la Dunia na kisha akashika namba mbili kwenye tuzo ya Ballon d’Or. Moore kilikuwa kipaji kikubwa sana kuwahi kutokea kwenye soka la England hasa kwa timu ya West Ham United na ndio maana klabu hiyo iliamua kufanya tukio la heshimu la kuistaafisha jezi yenye namba sita mgongoni kutokana na heshima yao kwa mchezaji huyo.

Johan Cruyff (Ajax #14)
Jezi namba 14 itakuwa ina maana moja tu kwenye mchezo wa soka na maana yenyewe ni Johan Cruyff. Klabu ya Ajax imeamua kuheshimu namba hiyo kwa kutoitoa kwa mchezaji yeyote kuivaa tangu msimu wa 2007/08. Kutokana na hilo, beki wa kati Thomas Vermaelen atakuwa mchezaji wa mwisho kuvaa jezi hiyo yenye namba 14 alipokuwa kwenye kikosi cha Ajax na hivyo sasa haitaonekana kwenye mgongo wa mchezaji mwingine katika kikosi hicho cha Amsterdam. Cruyff ni mchezaji mwenye heshima kubwa sana huko Ajax na Barcelona.

Mathieu Valbuena (Marseille #28)
Jezi yenye namba 28 iliyokuwa ikivaliwa na Mathieu Valbuena huko kwenye kikosi cha Olympique Marseille ilistaafishwa kwa muda baada ya mchezaji huyo kuondoka kwenye kikosi hicho mwaka 2014. Lakini, kitu ambacho Valbuena alikifanya kuwatibia Marseille ni pale alipoamua kujiunga na wapinzani wa timu hiyo, Olympique Lyon alipoamua kurudi tena kwenye soka la Ufaransa. Jambo hilo liliwafanya Marseille kuirudisha kwenye matumizi jezi hiyo yenye namba 28 mgongoni kutokana na uamuzi wa Valbuena, ambao hakuwaonyesha heshima waajiri wake waliojaribu kumpa heshima.

Ferenc Puskas (Honved #10)
Tuzo ya Bao Bora la Fifa imepewa jina lake kwa heshima kubwa kwa mchezaji huyo. Hakika Ferenc Puskas alikuwa staa matata kweli kweli kwenye enzi zake za kiuchezaji na kama kuna kitu alikuwa akikifanya kwa ufasaha mchezaji huyo basi ni kutumbukiza mipira kwenye nyavu. Alifanya makubwa sana katika klabu ya Budapest Honved. Katika mechi zake zaidi ya 300 alizocheza kwenye kikiosi hicho alifunga mabao ya kutosha, akiwa na rekodi ya kila mechi bao na ndiyo maana klabu yake ilichokifanya kwa heshima ni kuistaafisha jezi yenye namba 10 mgongoni.

Roberto Baggio (Brescia #10)
Roberto Baggio alijiunga na Brescia kwenye umri mkubwa kwenye maisha yake ya kisoka, alifanya hivyo akiwa na umri wa miaka 33 mwaka 2000. Wengi waliamini amekwenda kuvutavuta siku za kustaafu tu kwenye kikosi hicho, lakini Baggio alifunga mabao 45 katika mechi 95 alizochezea timu hiyo kwenye Serie A na kuwasaidia Brescia wasishuke daraja kwa misimu yote minne aliyokuwa kwenye timu hiyo. Kwa hilo alilowafanyia, Brescia waliamua kuistaafisha jezi namba 10 kwa heshima yake na haijawahi kuvalia tangu Baggio alipoondoka kwenye timu hiyo.

Daniel Jarque (Espanyol #21)
Mwanasoka mwingine aliyefariki dunia akiwa na umri mdogo sanna. Jarque alikuwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Hispania ya walio na umri wa chini ya miaka 19 na kushinda ubingwa wa Ulaya, sambamba na akina Andres Iniesta na Fernando Torres. Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 26 baada ya kupatwa na shambulio la mshtuko wa moyo, ikiwa ni mwezi tu tangu alipochaguliwa kuwa nahodha wa Espanyol. Kutokana na hilo, klabu yake iliamua kuistaafisha jezi hiyo kwa heshima ya Jarque, ambaye alikuwa swahiba mkubwa wa Iniesta.

Davide Astori (Fiorentina #13)
Mapema mwaka huu, ulimwengu wa soka ulikumbwa na mshtuko mkubwa baada ya kifo cha beki wa kati wa FIorentina, Davide Astori. Kutokana na heshima kubwa kwa nahodha wao huyo, Fiorentina waliamua kuistaafisha namba ya jezi aliyokuwa akivaa beki huyo kwa heshima. Kulikuwa na taarifa pia kwamba Fiorentina ilichukua uamuzi hata wa kuubadilisha jina uwanja wao wa mazoezi na kuitwa Sports Centre Davide Astori kwa heshima ya mchezaji huyo.