Kumbe siri ya Taifa Stars Uganda ni hii!

Sunday September 9 2018

 

By Majuto Omary

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe ameliomba benchi la ufundi la timu ya soka ya Tanzania 'Taifa Stars' kuendelea kuchagua wachezaji wenye moyo wa kuleta matokeo mazuri katika mashindano ya kimataifa.

Mwakyembe amesema hayo baada ya matokeo ya suluhu ya Taifa Stars dhidi ya timu yataifa ya Uganda 'The Cranes' katika mashindano ya kutafuta tiketi ya kufuzu fainali za Afrika (AFCON) Jumamosi iliyopita.

Waziri Mwakyembe amesema, wachezaji wasiokuwa na mapenzi na moyo wa kuiletea Taifa Stars matokeo mazuri hawana nafasi ya kuichezea timu hiyo.

Amesema, matokeo ya suluhu dhidi ya Uganda ni mazuri kwa Tanzania kwani magwiji wa soka Afrika wameshindwa kupata matokeo hayo kwenye uwanja wa Mandela.

Nchi kama Misri ilishindwa kutamba dhidi ya Uganda katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja huo.

“Haya matokeo ni fundisho kubwa kwa wachezaji ambao wanadhani timu ya taifa ni sehemu ya kupotezea muda, nampongeza Kocha Mkuu, Emmanuel Amunike na benchi la ufundi kwa maamuzi ya kuchagua wachezaji wenye mapenzi na moyo wa kupigania nchi yao.

“Wachezaji lazima wajue kuwa mambo yamebadilika na timu ya taifa ni kubwa kuliko zote, unapopewa nafasi lazima uitumie vizuri, tuna wachezaji wengi wenye vipaji  wanaweza kuleta matokeo mazuri nchini,” alifafanua Mwakyembe.

Ameongeza na kusema, endapo hamasa iliyopo kwenye timu ya taifa kwa sasa itaendelezwa, anaamini Tanzania itafuzu katika fainali za Afrika mwakani.

“Uzalendo, malengo na moyo wa kujituma ndiyo siri ya matokeo mazuri kwa timu ya soka ya Tanzania 'Taifa Stars' dhidi ya Uganda. Wakati wa mashindano ya Chalenji, Tanzania Bara ilichagua wachezaji wenye majina kuiwakilisha, Zanzibar ilichagua wachezaji wasiokuwa na majina lakini walikuwa na nidhamu na moyo wa kujituma, matokea yake, Tanzania Bara ilishindwa na Zanzibar kufanya vizuri, naomba kocha na viongozi waendeleze haya, hatuna haja na wachezaji wanaotukwamisha,” alisema.

Advertisement