Kumbe ishu ni Aussems tu

Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems

Muktasari:

  • TANGU aliyekuwa Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma atimke Msimbazi nafasi yake bado haijazibwa, lakini Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Patrick Aussems ameweka wazi ishu nzima ya msaidizi wake kwa sasa klabu ikijiandaa na mechi za kimataifa.

KIKOSI cha Simba, leo Ijumaa kitashuka Uwanja wa Taifa kuvaana na Big Bullets ya Malawi, lakini imefichuka kwamba Kocha Mkuu wa timu hiyo, Patrick Aussems ndiye aliyeshikilia tiketi ya Kocha Msaidizi wa kuziba nafasi ya Masoud Djuma.

Simba itacheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa na Wamalawi hao kama sehemu ya kujiandaa na mechi yao ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mbabane Swallows, huku ikiwakosa baadhi ya nyota wake wa kikosi cha kwanza.

Katika mchezo huo, Simba iliyopo nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara nyuma ya vinara Azam FC, itaongozwa na Kocha Aussems na yule wa makipa tu, Mharami Mohammed ‘Shilton’ kwani Mtunisia Adel Zrane hayupo nchini.

Kocha huyo wa viungo ambaye alikuwa akifanya kazi kama msaidizi wa Aussems tangu Mrundi Masoud Djuma atimuliwe amesafiri na anatarajiwa kurejea nchini alfajiri ya Jumapili ili kuanza maandalizi ya mechi ya kiporo cha ligi dhidi ya Lipuli.

Lakini wakati Zrane akirejea Jumapili, inaelezwa kuwa Mbelgiji wa Simba ndiye anayesubiriwa kwa sasa na mabosi wake ili kupendekeza jina la Kocha Msaidizi wa kuchukua nafasi ya Masoud, huku mwenyewe akidai hana tatizo kikazi.

MSIKIENI MWENYEWE

Kocha huyo aliyeiwezesha Simba kushinda mechi nane kati ya 12 na kupoteza moja tu, huku mbili wakitoka suluhu katika Ligi Kuu, alisema kwa mechi za kirafiki kwake haina shida kufanya kazi mwenyewe, ndio maana amempa Zrane mapumziko ya siku tano ili kwenda kuisalimia familia yake.

Alisema Mtunisia huyo atakuwa pamoja naye mazoezi ya Jumatatu ya kujiandaa na mchezo wao wa kiporo dhidi ya Lipuli utakaopigwa Jumatano kabla ya kuikaribisha tena Biashara United Novemba 25 na baadaye Mbabane Swallows.

Kuhusu kocha msaidizi wa kuchukua nafasi ya Masoud, alisema halina haraka kwake kwani kwa kipindi hiki anafanya kazi vizuri kwa kusaidiana na wasaidizi wake Zrane, Shilton na wengine waliopo benchi.

“Kwangu naona nafanya kazi bila ya tabu, hivyo kocha mwingine mpya msaidizi kwa sasa sio jambo la haraka, kwani niliokuwa nao katika benchi tumekuwa tukifanya kazi hiyo vizuri na maelewano makubwa kama nitakavyo,” alisema.

“Kama itatokea nitakuwa nahitaji msaidizi mwingine mpya nadhani labda katika mechi za mbele huko na nitaueleza uongozi ili uweze kulifanyia kazi hili,” alisema Aussems aliyejiunga na Simba kuchukua nafasi kutoka kwa Pierre Lechantre.

MRATIBU NAYE

Mratibu wa Simba, Ally Abbas alisema kuhusu suala la kocha mpya mwingine msaidizi atayechukua nafasi ya Masoud mapema kwani viongozi waliongia madarakani ni wapya.

Alisema: “Sidhani kama suala hili lina haraka kihivyo kwani viongozi wapya walioingia madarakani watakaa chini ili kuangalia kocha wa aina gani msaidizi ambaye anaweza kuja kufanya kazi na Aussems.

“Aussems kama atakuwa na mahitaji zaidi ya msaidizi mpya nadhani atawasiliana na uongozi mpya kwani hilo lipo ndani ya bodi na watalifanyia kazi,” alisema.