Kumbe huyu Mourinho hakumtaka Paul Pogba

Muktasari:

  • Kwa kifupi kwa mujibu wa Parames Pogba yupo Man United kwa sababu za kibiashara.

MANCHESTER, ENGLAND.KOCHA wa Manchester United, Jose Mourinho amesema kamwe hajawahi kutaka kumsajili Paul Pogba.

Hilo ndilo ndilo linalodaiwa na Eladio Parames.

Parames, 69, ambaye amefahamiana na Kocha Mourinho tangu utotoni na alikuwa ofisa habari wa kocha huyo wakati walipokuwa huko Benfica.

Parames alisema Mourinho hakuwahi kuunga mkono usajili wa Pogba kutoka Juventus na jambo hilo lilifanywa na Man United ni kwa ajili ya nguvu ya kibiashara tu.

Parames alidai Pogba hakuwa chaguo la Mourinho katika mipango yake na mabosi wa Man United walimsajili mchezaji huyo kwa ajili ya kujiongezea nguvu kwenye soko ili kuvutia mikataba ya kibiashara.

Kwa kifupi kwa mujibu wa Parames Pogba yupo Man United kwa sababu za kibiashara.

Katika hatua nyingine, Kocha Mourinho amekiri straika Romelu Lukaku hakuwa mchezaji pekee ambaye alihitaji kuketi naye kitako na kuzungumza naye wiki za karibuni. Imeelezwa Mourinho alikutana na wachezaji wake kadhaa mmoja mmoja na kuzungumza nao ana kwa ana kutambua shida ipo kwenye nini kabla ya mambo hayajakuwa mabaya zaidi.

Lukaku mwenyewe aliweka wazi kuzungumza na kocha huyo, lakini Mourinho alisema si kitu anachoweza kukisema hadharani kama ameketi na wachezaji wake kujadili baadhi ya mambo. Man United jana Jumatano usiku ilitarajiwa kumenyana na Valencia katika mchezo wake wa mwisho kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya makundi huku wikiendi hii ikiwa na kibarua kizito cha kuikabili Liverpool kwenye Ligi Kuu England.