Kumbe Yaw Berko ni Yanga

Muktasari:

Berko ambaye alibatizwa baba mchungaji kutokana na mambo aliyokuwa anafanya ndani ya klabu hizo alisema, pamoja na kuwa na mapenzi na Yanga haikuwa sababu ya kumfanya ashindwe kutimiza wajibu wake Simba au ikitokea akapata kazi huko.

MLINDA mlango wa zamani aliyezichezea klabu za Simba na Yanga, Mghana Yaw Berko ameweka wazi pamoja na kucheza katika vikosi vyote hivyo humwambii kitu kwa vijana wa Jangwani.

Berko ambaye kwa sasa yuko kwao Ghana na baada ya kumaliza kucheza aliingia kwenye ukocha huku akifanya kazi ya kuhubir na akawa anafanya kazi na klabu iliyomlea ya Libert Professional FC ambayo amemaliza nayo mkataba.

“Kusema kweli niliyapenda maisha ya Yanga zaidi na ndio klabu ambayo nimecheza kwa kipindi kirefu na nilikuwa na kipindi kizuri tofauti na ilivyokuwa Simba. Iko wazi nitasema Yanga ni timu nzuri kwangu na naipenda.”

Alisema, hata sasa ikitokea amepata nafasi amerudi hapo kwa ajili ya majukumu yoyote atafurahia kutokana na maisha aliyoishi kabla.

Berko ambaye alibatizwa baba mchungaji kutokana na mambo aliyokuwa anafanya ndani ya klabu hizo alisema, pamoja na kuwa na mapenzi na Yanga haikuwa sababu ya kumfanya ashindwe kutimiza wajibu wake Simba au ikitokea akapata kazi huko.

Berko aliichezea Yanga kwa misimu miwili tangu alipojiunga mwaka 2009 akitokea Liberty Professionals na kuachana nayo mwaka 2012 akarudi kwao lakini 2013 alijiunga na Simba aliyoichezea kwa miezi sita.