Kumbe Yanga wanafeli hapa

HAKUNA utata kwamba wakati wa usajili kwenye Ligi Kuu Bara, Yanga ilitikisa na usajili ambao waliufanya hali ambayo iliwafanya mashabiki wao waende wenyewe uwanja wa ndege kuwapokea wachezaji.

Mbwembwe, kelele na shangwe zilisikika kila kona na kuwafanya wapinzani wao kutulia, lakini ligi ilipoanza mwendo wao umekuwa wa kusuasua tofauti na matarajio ya mashabiki wengi.

Sio kwamba Yanga haipati ushindi, tatizo ni kwamba ushindi ambao wanaupata ni mdogo baada ya kucheza mechi tatu, wakishinda mechi mbili na kufunga magoli matatu wakiruhusu kufungwa goli moja.

Kocha Zlatko Krmpotic anasema anataka wachezaji watumie vizuri nafasi wanazozitengeneza, lakini jambo kubwa analofurahia ni kuona timu ikifunga.

“Tunatakiwa kutumia kila nafasi ambayo tunatengeneza, bado kuna kazi ya kufanya kuhakikisha mambo yote yanakuwa sawa, wachezaji kufunga zaidi kwenye mechi,” anasema kocha huyo ambaye baadhi ya wadau wanadai ameshindwa kuiunganisha timu.

Edo Kumwembe ambaye ni miongoni mwa wachambuzi wa masuala ya soka, anasema hajaelewa falsafa ya kocha huyo na kwamba mechi alizoangalia amekuwa akiona zaidi uwezo binafsi wa wachezaji.

“Sijaelewa falsafa ya kocha mpaka sasa, naona timu inabutua tu mipira mirefu, haitulizi mpira chini ikacheza pasi zinazoonekana, yaani mpira ukitoka kwa beki umeshapigwa mbele kule kwa mastraika,” alisema.

Herry Morris, mshambuliaji wa zamani wa Yanga na Prisons alisema: “Ubinafsi katika ufungaji ndio changamoto, yaani kila mshambuliaji anakuwa anataka kufunga, ukiwa mshambuliaji unaweza pia kutengeneza nafasi hata mechi iliyopita tuliona pasi aliyopata Mukoko Tonombe na kufunga haikuwa uchoyo ile.”

Kocha wa zamani Yanga na Bandari - Mtwara, Kennedy Mwaisabula, alisema awali alishawashauri mashabiki wa timu hiyo kukipa muda kikosi chao ili kuja kupata matokeo mazuri kutokana na timu kuwa bado ni mpya.