Kumbe Thomas Ulimwengu bado kidogo tu

Monday January 14 2019

 

By Eliya Solomon

KUMBE kwa mshambuliaji wa Kitanzania, Thomas Ulimwengu ni suala la muda tu kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha JS Saoura ambacho kimepoteza mabao 3-0 mbele ya Simba katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

JS Saoura imekiona cha mtema kuni Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwa kukutana na kipigo hicho, ambacho mabao yake yalifungwa na, Emmanuel Okwi na Meddie Kagere.

Kocha wa JS Saoura, Nabil Neghiz alisema pamoja na uzoefu wa kutosha alionao Ulimwengu anahitaji muda ili kuendana na soka lao pamoja na kuelewana kiuchezaji na wenzake.

“Ulimwengu ni mchezaji mzuri ambaye naamini atatusaidia kwenye michezo inayofuata, anahitaji muda ili kutuzoea kwasababu hana muda mrefu tangu ajiunge nasi,” alisema Nabil.

Mchezo dhidi ya Simba ni wa pili kwa Ulimwengu kuichezea JS Saoura katika mechi hiyo, nyota huyo wa kimataifa wa Tanzania, aliingia dakika ya 55 kuchukua nafasi ya Younes Koulkheir.

Ulimwengu aliichezea JS Saoura kwa mara ya kwanza mchezo wa Ligi Kuu Morocco, Januari 4 dhidi ya Kabylie ambapo timu hiyo ilipoteza kwa bao 1-0 kwenye uwanja wake wa nyumbani wa du 20 Août 1955 mjini Bechar.

REKODI YATIBUKA

Akiwa na TP Mazembe ya DR Congo, Ulimwengu alirejea nchini Juni 28, 2016 kwa mara ya kwanza akiwa na timu kutoka nje kucheza mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Yanga.

Katika mchezo huo, Ulimwengu aliiongoza Mazembe kuitandika Yanga bao 1-0.

Rekodi ya Ulimwengu kuja nchini na kuondoka na pointi tatu imetibuka safari hii kwenye michuano hiyo ya kimataifa kutokana na kipigo ilichokumbana nacho cha mabao 3-0.

Advertisement