Kumbe Sancho sio dawa Man U

MANCHESTER,ENGLAND. STRAIKA wa zamani wa timu ya Taifa ya England na Manchester United, Andy Cole amesema Man United haiwezi kuwa bora kwa kumsajili Jadon Sancho pekee na amesisitiza klabu hiyo itahitaji kusubiri kwa muda mrefu ili kurudi kwenye kiwango ilichowahi kuonyesha hapo awali.

Cole anaamini miamba hiyo ya Old Trafford itahitaji kusubiri kwa miaka isiyopungua miwili au mitatu ili kufikia levo za Liverpool na Manchester City kwa sasa.

Man United ambayo inatamani saini ya Sancho katika dirisha hili imefeli kufikia makubaliano na Dortmund ya kuilipa Pauni 109 milioni ambayo ndio ada ya mchezaji huyo wa timu ya Taifa ya England.

United ambayo wikiendi niliyopita ilikuwa inaanza ligi na ikapoteza kwa kipigo cha mabao 3-1, imekuwa na kiwango kibaya kuanzia msimu uliopita na msimu huu.

“Tuwe wa kweli, Man United inahitaji kusubiri kwa miaka miwili au mitatu ili kushinda taji la Ligi Kuu, hii ni kutokana na kundi kubwa la watoto ambao wapo kwenye timu, siamini kwamba kama Sancho atatua pale ndio watafanikiwa kuchukua ubingwa, ukiangalia Liverpool na Man City ambazo zina timu bora, zimesajili wachezaji wawili ambao ni bora,” alisema Cole.

“Mpaka Liverpool kuonyesha kuwa na timu ile yenye kiwango bora imewachukua miaka 30 na walisajili wachezaji wengi ambao pia walishindwa kufanya chochote,” aliongeza.

Cole pia alitoa mfano wa Man City ambayo ilisubiri kwa miaka 40, mpaka kuchukua ubingwa na ikiwa ilisajili wachezaji wengi katika kipindi chote hicho.

“Sikatai kuwa Sacho akija anaweza kuongeza kitu, lakini siamaini kama ataifanya Man United iwe sawa na zile klabu mbili za juu ambazo zinasumbua kwa sasa,” alisema.

Man United ilimaliza nafasi ya tatu katika msimu uliopita na ilimaliza kwa tofauti ya alama 33 nyuma ya Liverpool ambayo ndio ilikuwa bingwa na alama 14 juu ya Man City.