Kumbe Perez kazingua ishu ya Zinedine Zidane

Muktasari:

  • Real Madrid kwa sasa hali yao imekuwa ngumu kwelikweli kwenye La Liga, ikiachwa pointi 10 na vinara Barcelona, huku chanzo kikubwa kikidaiwa kuondoka kwa masupastaa hao wawili waliokuwa muhimu huko Bernabeu.

MADRID, HISPANIA.ALIYEKUWA Rais wa Real Madrid, Ramon Calderon amesema Florentino Perez ndiye chanzo cha Zinedine Zidane kuibwaga timu hiyo mwishoni mwa msimu uliopita na sasa hali imekuwa mbaya Santiago Bernabeu.

Calderon alisema uamuzi wa Perez wa kumpiga bei Cristiano Ronaldo uliopangwa mapema ulimtibua Zidane na kuamua kuachana na timu hiyo. Zidane na Ronaldo wote waliachana na timu hiyo ya Bernabeu majira ya kiangazi mwaka jana, kocha akiachia ngazi na mchezaji akiuzwa kwenda Juventus.

Real Madrid kwa sasa hali yao imekuwa ngumu kwelikweli kwenye La Liga, ikiachwa pointi 10 na vinara Barcelona, huku chanzo kikubwa kikidaiwa kuondoka kwa masupastaa hao wawili waliokuwa muhimu huko Bernabeu.

Calderon, ambaye alikuwa rais wa Madrid kati ya mwaka 2006 na 2009 alisema yote hayo kayataka Perez kwa uamuzi wake wa kumuuza Ronaldo na kumwaacha Gareth Bale kwenye kikosi kitu ambacho Zidane hakukitaka kabisa.

“Zidane alisisitiza kumbakiza Cristiano na Bale ndio auzwe,” alisema Calderon na kuongeza. “Lakini, Perez amefanya kinyume chake. Zidane alitaka kuwa mtu mwenye kuwa na uamuzi kwenye timu juu ya nani asajiliwe na nani auzwe, lakini hilo lilishindakana, akaamua kuondoka. Ulikuwa uamuzi sahihi.”