Kumbe Ndondo wala halina mwenyewe

Muktasari:

Mwaka uliofuata 2016, Kauzu FC nayo iliondoka patupu baada ya kushuhudia taji hilo likibebwa na Temeke Market ambayo nayo ililitema kwa Misosi FC mwaka 2017.

WAKATI hatua ya robo fainali ya Ndondo Cup ikizidi kupamba moto, mashindano ya mwaka huu yameendelea kuwa nuksi kwa timu zilizowahi kutwaa ubingwa wa mashindano hayo.

Hadi sasa hakuna timu ambayo imewahi kutetea taji la mashindano hayo ambayo yalianzishwa mwaka 2014.

Abajalo ya Sinza ndiyo iliyoanza kutwa taji hilo mwaka 2014 lakini ikashindwa kulitetea mwaka 2015 ambapo lilichukuliwa na Kauzu FC.

Mwaka uliofuata 2016, Kauzu FC nayo iliondoka patupu baada ya kushuhudia taji hilo likibebwa na Temeke Market ambayo nayo ililitema kwa Misosi FC mwaka 2017.

Licha ya wengi kutegemea Misosi FC ingelitetea taji hilo, ilijikuta ikiondoka patupu mwaka 2018 baada ya ubingwa huo kwenda kwa Manzese United ambayo nayo mwaka huu imeshindwa kufurukuta baada ya kuishia hatua ya makundi.