Kumbe Mfalme!: Rafiki wa Samatta Genk afichua yote

Muktasari:

  • Megan, ambaye alianza kumshangilia Samatta kwa kukubali uwezo wake tangu akiwa Simba kwenye michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, anasema ni nadra kuona vurugu zikitokea kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Luminus Arena.

HUKO England kuna mashabiki wakorofi kibao lakini wanaosifika ni wale wa Newcastle United, Na stori yao iliyobamba ni miaka sita iliyopita wakati mashabiki 29 wa Newcastle United FC walipotiwa mbaroni kwa kufanya vurugu baada ya kufungwa mabao 3-0 na wapinzani wao, Sunderland, 2013.

Achana na hao, huko KRC Genk kwa Mbwana Samatta kuna mambo tofauti kabisa, kuna mashabiki waungwana tu, na miongoni mwao yupo Mtanzania, Jeff Megan.

Megan, ambaye alianza kumshangilia Samatta kwa kukubali uwezo wake tangu akiwa Simba kwenye michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, anasema ni nadra kuona vurugu zikitokea kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Luminus Arena.

“Nipo huku kwa miaka mitatu sasa, nimekuwa nikienda mara kwa mara uwanjani na kujichanganya na mashabiki wa KRC Genk ni watu poa na wanapenda amani,” anasema Mbongo huyo, ambaye amefunguka mengi ikiwemo namna alivyoanza kumkubali Samatta tangu wakiwa Bongo hadi Ubelgiji, pia ameelezea Wabelgiji wanavyompa heshima yake.

MAMBO YALIANZIA MORO

Megan anasema kwa mara ya kwanza alionana na Samatta mkoni Morogoro kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara na Simba ilikuwa ikicheza dhidi ya Mtibwa Sugar.

Baada ya Samatta kusajiliwa na TP Mazembe, ushabiki wa Megan kwa Simba ulipungua na akawa anaendelea na maisha yake mengine.

“Nilikuwa nikifanya mambo yangu huku nikimfuatilia kupitia simu yangu ya kiganjani na kwa kusoma magazeti ambayo mara chache yalikuwa yakiandika taarifa zake hasa alipokuwa akifunga Ligi ya Mabingwa Afrika,” anasema.

AKATANGULIA UBELGIJI

“Kilichotokea ni kama nilitangulia Ubelgiji maana wiki chache baadaye zikaanza kuwepo kwa taarifa Samatta anawindwa na Genk.”

Katika mchezo wake wa nne tangu Samatta ajiunge na KRC Genk, ndipo Megan alipokata tiketi kwa mara ya kwanza nchini humo kwenda kumwona Mtanzania mwenzake. “Nakumbuka alifunga bao lake la kwanza kwenye mchezo huo ilikuwa dhidi ya Club Brugge, alifunga bao la tatu, ambalo lilikuwa la ushindi kwenye matokeo ya mabao 3-2. “Wakati wachezaji wanaingia uwanjani nilishtuka kutomwona Samatta akiwa ameanza kwenye kikosi cha kwanza na ukiangalia nilikuwa nimeingia uwanjani kwa ajili yake.

“Nilijipa moyo pengine angeingia mwanzoni mwa kipindi cha pili haikuwa hivyo ila niliingiwa na faraja nilipomwona akipasha, wapo waliokuwa wakisemezana kuwa yule ndiye mchezaji wetu mpya.

UKARIBU UKAANZA KUIVA

“Nilijitahidi kutafuta nafasi ya kuonana naye na kwa bahati nzuri nilifanikiwa na nilipoongea Kiswahili mbele yake alitabasamu na kutambua nilikuwa Mtanzania mwezake. Tangu hapo tukaanza kuwa karibu,” anasema.

KIPENZI CHA WATOTO

Megan anasema watoto wadogo kwenye Mji wa Genk wamekuwa wakimpenda sana mshambuliaji huyo wa Kitanzania na mara tu baada ya kumwona akikatisha mtaani humkimbilia na kutaka kupiga naye picha.

Pamoja na kujitengenezea jina kubwa Ubelgiji, Samatta haishi kistaa kabisa nchini humo, hayo anasema Megan, ambaye amekuwa akipata muda wa kupiga naye stori mbili tatu akijichanganya pia na rafiki zake. “Samatta ni mwelewa sana, amekuwa akiendana na Wazungu kwenye matumizi ya muda, ukiweka mihadi ya kuonana naye atakuwa ndani ya makubaliano.

ANAIBEBA TANZANIA

“Kwa kiasi kikubwa Samatta amekuwa ikiibeba Tanzania, mara kadhaa amekuwa akipambana kuibeba bendera ya taifa letu, wengi wanaijua Tanzania kwenye mji wa Genk kwa sababu ya uwepo wake,” anasema.

AMPELEKA MAN UNITED

Moja kati ya vitu ambavyo Megan anatamani vitokee ni Samatta kusajiliwa na Manchester United kutokana na mapenzi makubwa aliyonayo binafsi na klabu hiyo yenye historia kubwa England. “Naipenda Manchester, United na hata Mbwana pia ni klabu anayoipenda, kama ningekuwa napanga mimi basi nadhani msimu ujao angeichezea United,” anasema

ATAHAMA NAYE

Megan anasema endapo Samatta akitua England ataangalia uwezekano wa yeye kuhamia nchini humo ili kuendelea kumsapoti kinara huyo wa mabao Ubelgiji.

AMPA NENO MSUVA

Anasema umefika muda wa Saimon Msuva kuondoka Morocco ili kwenda kucheza soka barani Ulaya maana siku zote Wazungu wamekuwa makini na umri wa wachezaji.

“Msuva alitakiwa kuwa Ulaya maana kwa hesabu za kawaida atatakiwa kupoteza sio chini ya miaka mitatu hadi miwili kuwaaminisha watu kupitia timu za daraja la kati kama ilivyofanya Samatta huku Ubelgiji au alivyofanya (Victor) Wanyama.

“Ni ngumu sana kwa wachezaji wa Afrika Mashariki kutoka moja kwa moja Afrika na kwenda kwenye ligi kama England, Hispania, Ujerumani na Ufaransa.”