Kumbe Matola, Makame siri ni hii

Muktasari:

Eneo la Sinza jijini Dar es Salaam ambapo unakutana na saluni ya Nevada inayomilikiwa na Chrispine Mdemu (Nevada Junior), ambaye katika kuhakikisha anaiteka biashara akakusanya vinyozi wenye koneksheni ya kuwanyoa watu wazito.

MOJA ya kitu kigumu kwa staa yoyote endapo anataka kwenda katika wingi wa watu ni kujua amevaaje au kichwani mpaka uso wake uko katika ubora gani.

Hili sio kwa watu wa muziki au hata wale wanamitindo, lakini changamoto hii inawakuta hata mastaa wa soka na hata wale wa siasa ambao, kila saa kama sio kukaa mbele ya watu basi wataonekana katika luninga.

Kujua hilo ghafla Mwanaspoti likaonyeshwa chimbo ambalo mastaa wengi hulitumia kutengeneza muonekano wao, ambapo hapo wanakuwa na vinyozi tofauti wanaosimamia shoo.

Eneo la Sinza jijini Dar es Salaam ambapo unakutana na saluni ya Nevada inayomilikiwa na Chrispine Mdemu (Nevada Junior), ambaye katika kuhakikisha anaiteka biashara akakusanya vinyozi wenye koneksheni ya kuwanyoa watu wazito.

Kufika hapo tukakutana na kinyozi wa kwanza huuyu ni Khamis Hussein maarufu kama Khamis Baba.

Ana muda gani katika kazi hiyo?

Hatua ya kwanza ikawa kujua kazi hiyo ya unyozi ameifanya kwa muda gani, ambapo hapa Khamis Baba anaanza kwa kuelezea: “ Kwa haraka haraka nina zaidi ya miaka saba, lakini sikuanzia hapa nilikuwa nafanya kazi katika saluni mbalimbali kisha nikatua hapa.

“Nimekuwa nikinyoa watu mbalimbali wanaokuja kama wateja, lakini ndani yake wapo wa makundi tofauti kama unavyouliza wapo viongozi wa serikali, wasanii wa filamu, wanamuziki, watangazaji na hata wachezaji wa mpira.

Wanamuziki gani anawanyoa?

“Wanamuziki wako wengi lakini baadhi ni kama Jux, Linex, Joh Makini na rafiki yake G Nako, Ommy Dimpoz hawa mara nyingi wamekuwa wateja wangu katika kuwanyoa kila mmoja na mtindo wake anaoutaka.

Kuna ugumu gani kuwanyoa?

“Ugumu unakuwa kama unamnyoa mara ya kwanza hapo lazima utajitahidi utulie ili kuhakikisha unafanya kile anachotaka kama unavyojua hawa ni watu wanaokutana na makundi makubwa ya watu sasa ukikosea kumnyoa unakuwa unaharibu.

“Ukishamnyoa mara moja basi hatua ya pili ni rahisi labda itokee akija tena aje na mtindo tofauti anaotaka, lakini wanakuwa na mtindo maalum.

“Kumbuka hao wasanii niliokutajia kila mmoja ana mtindo wake wa nywele, hivyo akishaniambia anakuja au nimfuate basi unaelewa haraka kipi unakwenda kukifanya

“Kikubwa ni umakini kwa sababu hawa ndugu zetu ni kioo cha jamii sasa ukishafanya makosa basi unamkimbiza kabisa, lakini binafsi nimeshazoea na ni wateja wakubwa siku zote.

Utofauti wa huduma ya nyumbani na saluni

“Utofauti upo, kwanza inategemea na wapi unamfuata kuna gharama kidogo unaweza kulipiwa usafiri. Unajua ukifanyia saluni hakuna mambo mengi tofauti na nyumbani unaweza kumuona labda kaingia chumbani sasa kuna suala la muda hapo utakuta anaamua kufidia.

Kumbuka nikikufuata nyumbani pia kuna wateja nawapoteza huku ofisini na wengi huwa tunafanyia sopu sopu nyumbani kwa sababu wanakuwa huru na hawapendi kuonekana onekana mitaani.

Amewahi kuwanyoa wachezaji gani wa soka?

“Wachezaji ni wengi Erasto Nyoni (Simba), Juma Abdul, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ Nchimbi aliyetupeleka fainali za CHAN, Tumba Swedi, Abubakar Salum ‘Sure Boy na hata Tambwe (Amissi).

Kuna wakati tunakwenda kuwanyoa katika timu zao hata klabuni wakiwa kambini, lakini pia kuna wakati tunawanyoa mmoja mmoja.

“Unajua wachezaji sio hawapendi kunyoa mara kwa mara changamoto kubwa imekuwa ni ratiba zao za kukaa kambini muda mrefu, lakini wakiwa likizo ndio huja mara kwa mara mfano hivi juzi tulilazimuika kuwafuata katika kambi ya timu ya taifa na tukawanyoa ambao hawana vinyozi maalum.

Samata, Msuva wana vinyozi wao bana

Tulipokwenda kambini Stars tuliwanyoa wachezaji wengi, lakini hatukubahatika kuwanyoa nahodha Mbwana Sammata na Simon Msuva wao walikuwa tayari wameshanyoa kwa vinyozi wao, lakini tunachofurahi huduma ambayo tuliwpaatia wenzao waliifurahia sana.

Mitindo ya wachezaji

“Wachezaji wengi wanapenda kunyoa panki na kuacha nywele kidogo juu wanaweza kuweka ‘dredi’ huu ndio mtindo wao mkubwa ni mara chache unaweza kukutana na mchezaji akataka kumnyoa kawaida tu halafu aondoke.

Kwanini mtindo huo?

“Niliwahi kuwauliza kama wachezaji wawili hivi kwanini wanapenda mtindo huu wakaniambia sababu kama inalingana kwamba, wakiacha nywele kidogo zinawasaidia wanapokuwa uwanjani wanaporuka juu kuwania mpira.

“Unajua wachezaji huwa wanaumizana wakati mwingine ni kwa makusudi sasa wakasema wakiwa na nywele mtu hata akimpiga kiwiko hawezi kuumia sana labda apigwe usoni, lakini kama ni kichwani inakuwa ni nafuu kidogo.

Vipi kuhusu makocha na mitindo yao

“Makocha ni tofauti kidogo wao hawapendi kunyoa kama wachezaji unaweza kukuta kocha kama Matola (Seleman) ananyoa nywele zote kichwani na ndevu zake ana mtindo wake wa kuziachia na kuzichonga, kocha Ettiene (Ndayiragije) ananyoa kawaida tu ana anapendeza vizuri.

Tukiachana na Khamis Baba kinyozi mwingine Aidan Juma, ambaye ni kiongozi katika kundi la vinyozi hao naye anayelezea kazi yake hiyo kwa kuwanyoa watu maarufu

Wanasiasa wakiingia saluni inakuaje

“Unajua unapowanyoa wanasiasa hawapendi vurugu wala makelele mara nyingi wanapenda utulivu na kuona watu wanajiheshimu.

“Mara nyingi hapa kwetu akiingia mwanasiasa tu hali hubadilika utaona hata kama tulikuwa tunataniana ghafla utulivu hutawala na kila mmoja anakwenda kukaa sehemu yake. Labda itokee yeye ndio aanzishe utani basi na wewe utachangia kidogo na kwa nidhamu.

Huleta stori za kisiasa?

“Hapana unajua hapa kwetu wanakuja watu tofauti wa siasa kuna wengine wa CCM, Chadema na wakija kila mmoja huwa na habari zake kama utani unakuwa wa kawaida kuhusu maisha. Labda Jerry Murro ndio ataingiza utani wa mpira kidogo kama kawaida yake akimaliza anaondoka zake.

Wanasiasa wengine ambao hupenda chimbo hilo ni Meya wa Ubungo, Steven Jacob na Khamis Baba anafichua kwamba, aliwahi kumnyoa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati kabla hajapewa wadhifa huo.

HAPA ALIKOMESHWA

“Msanii ambaye huwa akija kunyoa anatumia muda mrefu ni Rayvvan, ambaye mara zote huduma zake ni nyingi anaweza kutumia hata saa mzima akiwa saluni hadi akitoka mwenyewe unakubali kuwa, jamaa kawaka.

“Kuna wakati niliwahi kumhudumia mcheza kikapu Hashim Thabit, nilipata shida tena wakati huo alikuwa anatokea Marekani sasa zile wave za Marekani zilikuwa zimekolea sana, shida ikaja anataka kitu kama kile ilitupa shida.

Tulijitahidi kumtoa kama vile, lakini hakuwa akiamini na mwisho tulipomaliza alitupongeza kwani, alitokea kinoma japo kazi ilikuwa nzito kwelikweli.