Kumbe Man United bado wanamtaka Pochettino

LONDON, ENGLAND. MAURICIO Pochettino amerudi upya kwenye rada za Manchester United shukrani kwa klabu yake ya zamani, Tottenham Hotspur.

Spurs iliichapa Man United 6-1 Jumapili iliyopita kwenye Ligi Kuu England, huku miamba hiyo ya Old Trafford ikicheza soka la ovyo kabisa jambo linaloibua wasiwasi mkubwa wa kuhusu nafasi ya Kocha Ole Gunnar Solskjaer.

Kikosi cha Man United kimekumbana na kipigo kizito ikiwa nyumbani Old Trafford na kumekuwa na wasiwasi mkubwa huenda vichapo vingine vya aina hivyo vinaweza kuendelea.

Solskjaer, ambaye aliongoza Man United kushika nafasi ya tatu kwenye ligi msimu uliopita na kufika nusu fainali ya Europa League, kwa msimu huu kikosi chake kimesharuhusu mabao 11 katika mechi tatu tu ilizocheza kwenye ligi.

Kinachoripotiwa ni makamu mwenyekiti mtendaji, Ed Woodward anaanza kupiga hesabu za kunusuru hali ya mambo. Woodward hatamfukuza Solskjaer katika kipindi hiki cha mapumziko ya mechi za kimataifa.

Lakini, yeye ni shabiki mkubwa wa Pochettino na mabosi wengine wakubwa kwenye kikosi hicho cha Old Trafford wamekuwa wakiwasiliana na mawakala wa kocha huyo Mhispaniola.

Pochettino, ambaye aliiongoza Spurs kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 2019, kabla ya kufukuzwa Novemba mwaka jana ameweka wazi dhamira yake ya kutaka kurudi kwenye ukocha.

Kocha huyo (48) amekataa ofa za klabu kibao, ikiwamo ya Benfica ya Ureno na aliwahi kuhusishwa na Barcelona. Lakini, ameamua kutulia akisubiri timu yake anayoitaka kuinoa.

Kocha Pochettino ni mkali wa kufanya kazi na wachezaji vijana, hivyo akitua Man United hatakuwa na tatizo kutokana na kikosi hicho kusheheni vijana wengi wenye vipaji vikubwa.