Kumbe Lionel Messi ameruhusiwa kuhama

Muktasari:

Messi tangu amejiunga na Barcelona akiwa mtoto hajawai kucheza timu yoyote na mafanikio yake yote ameyapata akiwa na miamba hiyo ya Hispania

BARCELONA, HISPANIA. Kama wewe ni Manchester City au Manchester United na timu nyingine zenye viwango hivyo, ukiisaka saini ya supastaa wa Barcelona, Lionel Messi basi utasubiri sana.

Unajua kwanini? Messi anaweza kuuzwa na Barcelona miaka miwili ijayo, lakini shida ni kwamba hilo likitokea, basi hawezi kupelekwa kwenye klabu kubwa au yenye upinzani kwa wababe hao wa Nou Camp.

Taarifa zinafichua kwamba kwenye mkataba wa Messi huko Barcelona kuna kipengele kinachoruhusu mchezaji huyo kuondoka itakapofika mwaka 2020.

Wakati mkataba wake wa sasa ukifika tamati 2021, Mundo Deportivo linaripoti kwamba mabosi wa Barcelona wapo tayari kumwongezea mwaka mmoja Messi ili abaki kwenye kikosi chao hadi Juni 2022.

Lakini, kipengele kilichowekwa kwenye mkataba wake kinamruhusu kuondoka itakapofika 2020, kwa sharti moja tu kwamba asiende kujiunga na klabu kubwa ya Ulaya.

Messi alisaini mkataba wake wa mwisho kwenye kikosi hicho cha Barcelona, Novemba 25, 2017, ambapo mkataba huo utakwenda hadi Juni 2021. Kwenye mkataba huo ndio kuna kipengele kunachomruhusu kuondoka Juni 2020.

Wakati rais wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu akiwa tayari kuheshimu kipengele hicho, anamtaka Messi pia kuzingatia makubaliano hayo yaliyopo kwenye mkataba kwa maana kwamba asitue kwenye timu yoyote kubwa kama ataamua kuachana na wababe hao wa Catalan. Man City iliwahi kuripotiwa kumtaka Messi na kwamba ilimwaandilia mshahara mara tatu ya anaolipwa huko Barcelona kitu ambacho kingemfanya Muargentina huyo awe analipwa zaidi ya Pauni 1 bilioni kwa wiki.