Kumbe Kocha wa Kaseja ni mwanamama!

UNAPOMKUTA kwenye majukumu yake uwanjani wengi hushangaa inakuwaje anamudu kuwanoa vidume wakati ni mwanamke. Lakini mwenyewe anakuambia “Hapa kazi tu”. Na ukimleta dharau naye anakuzingua kwani anasimamia sheria na kile anachokiamini.

Namzungumzia Fatuma Omari, kocha wa makipa timu ya Ligi Kuu Bara, KMC yenye makipa wanne akiwemo mkongwe Juma kaseja.

Alipataje Nafasi

Fatuma anasema ubora wake ndio ulimpeleka KMC kutokana na uongozi wa timu kuvutiwa na uwezo wake. “Mara ya kwanza nilikuwa naenda pale kwenye Uwanja wa Bora Kijitonyama ambako KMC walikuwa wanafanyia mazoezi na niliomba kufanya nao mazoezi tu wakati huo kocha wa makipa akiwa ni Riziki Shawa.

“Baadaye ligi ikasimama kwa miezi mitatu kutokana na corona na iliporejea nikaendelea na mazoezi na timu huku pia nikimsaidia baadhi ya kazi kocha Shawa.

“Wakati naendelea nao viongozi wakapenda utendaji wangu wa kazi na wakaniambia kama nina vyeti nipeleke ofisini na nikafanya hivyo, kwani nimesomea hii kazi,” anasema Fatuma.

Anasema wakati huo Shawa alikuwa na tatazo la goti lililosababisha ashindwe hata kupiga mpira, hivyo akapumzika na yeye kupewa nafasi hiyo ambayo yuko nayo mpaka sasa.

Makipa wote KMC wanamuheshimu

Usifikiri kama kuwafundisha wanaume, basi makipa wanamdharau, la hasha kwani mwenyewe anakuwambia wote wanafuata mafunzo yake vizuri.

Fatuma anasema hakuna kazi anayoifurahia kama hiyo kwa kuwa hupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa makipa hao, wakiongozwa na Kaseja. “Niko huru na naifurahia kazi yangu. Sijakutana na changamoto yoyote, labda huko mbele, ila sidhani kwani hata zikitokea nitajua jinsi gani ya kuzikabili.

“Nashukuru makipwa ninaowafundisha wakiongozwa na Kaseja wananisikiliza kama kocha wao,” anasema Fatuma.

Wachezaji wote hawawezi kunidharau kwa sababu lazima watajiuliza kipa mzoefu kama Kaseja ambaye ana wafuasi wengi (anamheshimu), lakini ninapokuwa mazoezini au uwanjani ananisikiliza, ananiheshimu iweje wengine wasiniheshimu.

KMC, timu za Taifa anajigawaje?

Fatuma anasema licha ya kuwa kocha wa makipa wa KMC, pia ni kocha wa makipa wa timu zote za Taifa za wanawake ikiwemo ya chini ya miaka 17, 20 na ya wakubwa. “Kweli huwa nafundisha na timu za Taifa, lakini tangu nimeajiriwa KMC hakujatokea mashindano kwa soka la wanawake, hivyo naamini hata kwa sasa kukitokea mashindano yoyote, basi mamlaka husika zitaongea na mabosi wangu na nitafanya kazi katika sehemu ambayo watakubaliana,” anasema.

Makocha wengi hawajasoma

Baadhi ya timu za Ligi Kuu zina makocha wa makipa huku nyingine wakitumia ujanja ujanja tu kuwaweka watu ambao hawana uzoefu na kazi hiyo, jambo ambalo Fatuma anakiri kuwa kweli kuna uhaba mkubwa wa makocha waliosomea kozi ya ukocha wa makipa.

“Naamini kozi zikiendelea kuja na watu wajitokeze kwenda kusoma kwani ni muhimu na itawaongezea ujuzi zaidi na watakuwa wanaenda kusawazisha makosa ya makipa wao kwenye timu zao,” anasema Fatuma ambaye amesoma kozi ya ukocha wa makipa kwa ngazi ya ‘advance’ mwaka 2016 huku pia akiwa amesomea zile za awali za ukocha wa kawaida.

Tatizo la makipa

Fatuma anasema tatizo kubwa la makipa nchini ni kutokaa katika nafasi zao.

“Wengi hawajui jinsi ya kukaa katika nafasi. Hawaelewi mpira uko wapi na anatakiwa kuwa wapi na kwa wakati gani, jambo linalosababisha wakati mwingine kufungwa mabao ambao yangeweza kuzuilika.”

Kinachomkera

Kuna kipindi kipa wa Simba, Aishi Manula aliingia katika lawama kutoka kwa mashabiki wakimlaumu kufungwa mabao ya mbali, lakini pia si yeye tu kwani hata makipa wengi kwenye ligi wamekuwa wakiingia katika lawama timu zao zinapopoteza mechi, jambo linalomuumiza Fatuma.

“Najisikia vibaya sana kwa nini watu wengi huwa wanapenda kuwalaumu makipa wakati mwingine bila sababu,” anasema.

“Mpaka ukiona kipa kafungwa bao la mbali ina maana hakupata ushirikiano mzuri kutoka kwa wachezaji wenzake, kwa sababu kama wangesaidia kumdhibiti mfungaji kipa asingefungwa mabao. Lakini kwa sababu Watanzania tunapenda kulaumu, pia tunapenda matokeo mazuri tu na kusahau kuwa mpira una matokeo matatu, kushinda kufungwa na kutoka sare.

“Mchezaji yeyote anaweza akafanya kosa katikati ya uwanja linalosababisha kipa akafungwa, lakini watu wengi mara nyingi wanapenda kuangalia tukio la mwisho na ndipo hapo wanaposhusha lawama nyingi kwa kipa na kusahau kosa lilipoanzia.”

kuolewa badobado

Fatuma ambaye ana mtoto mmoja aliyemzaa akiwa kidato cha nne, anasema hana mpango wa kuolewa kwa sasa licha ya kukiri kuwa na mchumba.

“Mchumba ninaye, ila kwa sasa sitamani kuolewa kwa sababu bado natafuta maisha.Ngoja kwanza nijipange,” anasema.

“Maisha yenyewe ya sasa sio vizuri kuharakishia ndoa kwa sababu kuna wengi wapo kwenye ndoa wanatamani kutoka na wengine wanaifurahia. Kuna wengine wanapata tabu, lakini wanakomaa nayo mpaka wanapoteza maisha, hivyo bado nipo nipo sana.”

Historia yake

Kocha huyo anasema awali alikuwa akicheza nafasi ya ushambuliaji timu ya Chadamali Queens iliyopo mkoani Ruvuma na baadaye akatua Sayari Queens ya Dar es Salaam.

“Nilikuwa mshambuliaji mzuri tu wakati nipo kwetu Ruvuma, lakini baadaye nikaona nimechoka kukimbiakimbia uwanjani ndio nilimfuata kocha kipindi hicho Sayari Queens, anaitwa Juma Bomba nikamwambia nitashindwa kutimiza ndoto zangu hivyo naomba kuhamia golini na unifundishe ukipa.

“Akasema haina shida kama una nia na malengo freshi, hivyo akaanza kunifundisha.” Mpaka sasa anasema uwezo wa kudaka anao.”