Kumbe,Kibadeni alitoswa Yanga ndio akatua Simba

Muktasari:

  • Mwanaspoti lilifika nyumbani kwa kocha huyu mwenye historia na rekodi matata kabisa kwenye soka, pale Sinza kwa Remmyi na kupiga naye story ambazo hakuwahi kuzifichua hapo awali. Kibaden amefunguka mazito ikiwemo majina ambayo anatumia kuwa ni feki.

KABLA ya Abdallah Kibaden ‘King’ kutua Simba kwa mara ya kwanza mwaka 1970, alianzia Yanga ambako alikuwa anafanya mazoezi na timu hiyo, lakini hakuna aliyekiona kipaji chake kwa wakati huo na kumfungulia mlango.

Unaambiwa straika huyo mweny umbile dogo na mwepesi wa kupenya mabeki enzi zake alikuwa akienda Uwanja wa Kaunda pale Jangwani kufanya mazoezi.

Kikubwa alitarajia angeweza kuvaa jezi za Yanga ili aitumikie timu hiyo, lakini mipango yake ilikwamishwa.

Kibaden anafichua kitu hicho ambacho kilimfanya kwenda kufanya mazoezi na Yanga mwaka 1969 kuwa ni kuvutiwa na sana na rangi za jezi zao kwa kuwa zimefanana na zile za Chama Cha TANU ambapo ndani ya familia yake ni wapenzi wakubwa wa chama hicho.

Baba yake mzazi aliyemtaja kwa majina ya Athuman Seifu, miaka ya 60 alikuwa Mwenyekiti wa TANU, akaja kuwa diwani wa CCM Wilaya ya Ilala, hivyo rangi za njano na kijani zilitawala nyumbani kwao na hilo likamfanya avutike mpaka Jangwani ambako wanatumia jezi zinazoendana na rangi hiyo.

Mwanaspoti lilifika nyumbani kwa kocha huyu mwenye historia na rekodi matata kabisa kwenye soka, pale Sinza kwa Remmyi na kupiga naye story ambazo hakuwahi kuzifichua hapo awali. Kibaden amefunguka mazito ikiwemo majina ambayo anatumia kuwa ni feki.

HUYU HAPA KIBADEN HALISI

Majina yake halisi aliyopewa na baba yake mzazi ni Abdallah Athuman Seifu, mwaka 1959-1962 wakati akisoma Shule ya Msingi Habibu Punja Muslim, iliyopo Ilala, Dar es Salaam.

Wanafunzi wenzake walimtunga jina la Kibaden, akiwa darasa la pili.

Jina la Kibaden lilitokana na nyimbo waliokuwa wakiimba wanafunzi wanzake ‘Abdallah Kibaden kanya mavi mtendeni kamsingizia mgeni’ ndipo wakampachika yeye, lakini anasema mzee wake, Athuman Selfu alikuwa hapendi hata kulisikia jina hilo.

Lakini jina hilo likavuma sana na kulazimika kubadili hata kwenye vyeti vyake vya shule.

“Badala ya Abdallah Athuman Self, nikawa naitwa Abdallah Kibaden na hilo halikutokana na soka kama wengi wanavyodhani na mwisho wa siku baba iliamua kukubaliana na hali halisi kwani, hakuwa na namna ya kulizuia.

DAU LAKE SIMBA

Kibaden alijiunga na Simba mwaka 1970 ada ya usajili wake alipewa viatu vya kuchezea na jezi ya mazoezi. Kuhusu mshahara walimtafutia kazi katika Kampuni ya Filamu ‘Tanzania Film Company’ akiwa mkurugenzi wa ufundi.

“Zamani tulikuwa tunacheza soka baada ya kazi ndio maana tulikuwa hatuna mishahara katika timu. Pesa ikipatikana getini inakwenda kununua tofari za kujengea lile ghorofa unaloliona pale Kariakoo.

“Watanzania wajue wachezaji wa zamani tulitoa jasho letu katika jengo hilo. Pesa inayoitwa posho za wachezaji kwa sasa enzi zetu zilienda kwenye ujenzi, hivyo halikujengwa kirahisi kama baadhi wanavyodhani na kusahau mchango mkubwa wa wachezaji wa zamani,”anasema.

JINA KING NA PELE

Zamani wakati anacheza anasema Brazil ndiyo ilikuwa juu kisoka, mchezaji ambaye alikuwa anamuiga staili yake ya kucheza ni Edson Nascrimento ‘Pele’ Mfalme wa soka duniani, mashabiki walipoona kiwango chake ni cha kustajabisha walimuita King.

“Nikiwa Simba lilizaliwa jina la King, mashabiki wakinilinganisha na mfalme wa soka duniani Pele, kwa hiyo nikajikuta naitwa Abdallah Kibaden ‘King’,”anasema.

BATA ZA MASHABIKI

Anasema pamoja na kutopata posho wala mshahara, alikula neema ya nchini kw asana tu.

“Nilikuwa nikienda sokoni napewa samaki waliojaa kwenye kapu, vitunguu, nyanya yaani kila mtu anatamani nichukue vitu.

“Nilipanda bure daladala, nilijaziwa mafuta full tank kwenye gari langu nikipita sheli, nilichukua nguo bure dukani, nguo zangu zilikuwa zinafuliwa bure day cleaner nilikula vitu vingi vya mashabiki,”anasimulia.

MAHADHI APEWA KIWANJA

“Mwaka siukumbuki vizuri, Simba kulikuwa na makipa wawili matata, ilikuwa mechi ya Simba na Yanga, Mambosasa alimchokoza Omary Mahadhi tuliyekuwa tunamtegemea kwenye mechi hiyo, akasusa na kuondoka kambini.

“Hata mimi katika mechi hiyo sikumwamini Mambosasa kudaka mechi hiyo, dereva wa Simba Saleh Kambangwa alikuwa na uwanja, akaniambia nitampa kiwanja Mahadhi twende tukambembeleze acheze.

“Nikamfuata mpaka Magomeni tukamwahidi uwanja, akakubali akacheza baada ya mechi akakabidhiwa uwanja na hati yake, alijenga lakini watoto wake kina Wazir Mahadhi walikuja kuuza badaye,”anasema.

TUKIO LILILOMWACHIA KILEMA

Anasimulia miaka ya 70 alikuwa katika Hotel ya Holiday Inn ya Posta ambako walikuwa wanaweka kambi ya Taifa Stars, siku hiyo kulikuwa na tuzo, nilitoka mida ya jioni mpaka baharini, nilinunua dafu moja na soda nilishika mkononi, wakati naenda kwenye gari langu ambalo nilikuwa nimelipaki pembeni, niliona vijana wawili wamezipa nyoso zao na vitambaa.

“Walikuja kwa ajili ya kunizuru, wakati nataka kujikinga nikawapiga na chupa ya soka walikwepa, wakatoa panga na kunikata kidole, hawakuchukua kitu chochote, nilipoanguka wakaja Wahindi kunisaidia kunipeleka mpaka Hospitali ya Ocean Road, ikashindikana kunitibia nikapelekwa Muhimbili, zoezi la tuzo kwangu ikawa basi, mpaka leo sikujua kwa nini nilifanyiwa hivyo,”anasema.

BEKI WA YANGA WALIOMTESA

Kibadeni anashangaa kuona mabeki visiki kwa sasa wamebakia majina, anasema Yanga walikuwa na mabeki Boy Wikens ambaye alikuwa anavuta nywele zake na kuzitafuta kisha ananda kumkaba.

“Jamaa alikuwa anatisha alikuwa anakula nywele akikusogelea kukukaba lazima utumie akili nyingi kuvuka eneo lake, lakini pia kuna mtu alikuwa anaitwa Juma Shaban sifa yake kuu alikuwa anakukatia mtama kuanzia kiunoni ukinyanyuka wewe shujaa.

Katika kuthibitisha hilo, Kibadeni analiunganisha Mwanaspoti kwa njia ya simu na Juma Shaban.

Beki huyo naye anafunguka namna ambavyo Kibadeni alikuwa mwiba na walikuwa wanamfanyia mikakati ya kumkaba kuanzia mazoezini.

Stori na Kibaden zinakata kwa muda, mazungumzo yanahamia kwa Juma Shaban kwa muda.

“Unajua Kibaden alikuwa straika mwepesi wa kunyumbulika, anatumia akili sana kufunga hata njia ikiziba kiasi gani anapenya tu.

“Mfano siku akimkaba Wickens tunaanza kumlaumu mazoezini hivi kajamaa kanakushinda wapi, ukisikia straika hatari wa kucheka na nyavu, basi huwezi kuacha kulitaja jina lake,” stori beki hiyo inaishia hapo.

KIKOSI CHA SIMBA ANACHOKIKUBALI

Anasema makipa Athuman Mambosasa na Omary Mahadhi (wote ni marehemu), walikuwa wana ushindani mkali, hivyo walikuwa wanapangwa kutegemeana na mechi husika, beki namba mbili ni Shaban Balaza/ Daud Salum (marehemu), (beki wa kushoto) Mohamed Kajole/Khamisi Askari (marehemu), ( beki wa kati ni) Mohamed Bakari ‘Tall’.

Beki wa kusimama mwisho ni Aloo Mwitu, (kiungo) Athuman Juma/ Khalidi Abeid, (winga) Willy Mwaijibe, (kiungo wa juu) Khaidari Abeid, ( straika) Adam Sabu ( namba 10) Abdallah Kibadeni/Kessy Manangu na winga wa kushoto ni Abbasi Dilunga/Martin Kikwa.

Kibadeni amecheza mechi nyingi sana lakini kuna mechi hawezi kuisahau katika maisha yake ni ile yam waka 1977.

“Mechi ambayo ninayoikumbuka ni ile ambayo tuliifunga Yanga, mabao 6-0 rekodi ya hat trick yangu hiyo haijavunjwa hadi leo kutokana na vijana wengi kutojituma kisawasawa kwa ajili ya ajira yao, tofauti na zamani ilikuwa burudani.

“Siri kubwa iliyonifanya nijitume sana katika soka ni familia yangu ilikuwa maskini. Baba alikuwa mwenyekiti wa TANU, lakini pia diwani wa Ilala, akirudi kutoka kazini alikuwa anauza mkaa na magazeti ambayo wakati mwingine nikitoka mazoezini nilikuwa naenda mtaani kuyauza,” anasema.

Kuna mafanikio ambayo Kibadeni ameyapata akiwa Simba je, unayajua? Usikose Mwanaspoti kesho Ijumaa.