Kuishi Bongo kumemshinda mzungu wa Lyon

Muktasari:

Da Coasta amestajabishwa na wachezaji wa Bongo wanaofanya kazi kubwa, lakini wanachokipata ni kiduchi, jambo hilo kwa upande wake limeshinda akaamua kuachana na African Lyon na kurejea kwao Ufaransa.

MAISHA ya Bongo yamemshinda straika wa kimataifa wa African Lyon, Victor Da Coast baada ya kuona uongozi wa timu hiyo, umeshindwa kumlipa mshahara wa miezi miwili ameona isiwe tabu akaamua kurejea nchini kwao Ufaransa ili kuendelea na mambo mengine.
Da Coasta alijiunga na Lyon msimu huu, alipotua Tanzania alikuwa na matarajio makubwa ya kuendelea kisoka, lakini hakujua hali halisi ya uchumi wa timu yake mpaka alipoonja joto la jiwe kwa kukosa mshahara ndani ya miezi miwili.
Aliliambia MCL Digital kwamba amestajabishwa kuona wachezaji wana moyo wa kujituma licha ya kutolipwa mishahara yao, jambo ambalo kwa upande wake amedai limemshinda.
"Nimejifunza kitu kikubwa Tanzania hasa kwenye mambo ya soka, ili mchezaji aweze kufanya kazi nzuri lazima akili yake iwe imatulia, yasiwepo mambo mengine pembeni ambayo yanakuwa yanamfanya asiwe vizuri.
"Sasa ndani ya miezi miwili mchezaji hajui maisha yake yataendeshwa vipi, lakini anajituma kwa bidii kama vile kazi ya kujitolea, hilo limenistajabisha, sasa unajiuliza wanafanya kazi ya soka kwa ajili ya nini.
"Unafanya kazi ili uongeze kipato chako, lakini usipolipwa ina maana umeenda kupoteza muda, soka ni biashara kubwa Duniani kwa sasa, ila hapa Tanzania ninaona sivyo ndivyo,"anasema.
Da Coasta amasema baada ya kurejea nchini kwao, ataendelea na mazoezi huku akifanya shuguli nyingi za kumuingizia kipato.
Lakini alipoulizwa ndani ya kikosi chao ni mchezaji gani kukitokea timu kwao anastahili kucheza soka la Ufaransa! Da Coasta alijibu "Haruna Moshi 'Boban' ana ufundi mkubwa uwanjani nadhani akiamua kucheza nje ni mchezaji anaweza kufika mbali,"anasema.