Kuiona Simba, UD Songo buku tano tu mwanangu

Muktasari:

Simba inatakiwa kushinda mchezo huo ili kusonga mbele katika mashindano hayo baada ya mchezo wa awali uliofanyika Msumbiji timu hizo kutoka suluhu

Dar es Salaam. Mashabiki wa Simba watangaziwa kiingilio cha chini cha Sh 5000 kushuhudi mchezo wa marudiano wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika Kati ya Simba na UD Songo utakaochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akitangaza viingilio hivyo Afisa habari wa Simba, Haji Manara aliwataka mashabiki wa mabingwa hao kujitokeza kwa wingi uwanjani Jumapili.

Viingilio vingine katika mchezo huo ni Sh15,000 kwa VIP B na C, Platnum Sh 100,000 na Platnum + ni Sh 150,000.

Simba inatakiwa kushinda mchezo huo ili kusonga mbele katika mashindano hayo baada ya mchezo wa awali uliofanyika Msumbiji timu hizo kutoka suluhu.

Manara amewataka mashabiki wa klabu hiyo kufika kwa wingi Jumapili na kuujaza Uwanja ili  kuwapa sapoti wachezaji.

"Matarajio yetu ni kuona mashabiki 60,000 wanafika uwanjani na kuujaza Uwanja.

"Simba ina wachezaji wazuri na mastaa, lakini staa namba moja ni shabiki wa Simba.

"Kila mara tumekuwa tukitumia mtaji wa mashabiki wetu kuufanya Uwanja wa Taifa kuwa machinjio rasmi ya wapinzani wetu hivyo na Jumapili lazima tuendeleze hilo. Lazima tuhakikishe UD Songo anafungwa na tunasonga mbele.”