Kouyate: Mane wamemnyima Ballon d'Or kwa sababu ni Mwaafrika

Muktasari:

Mane aliongoza Senegal kumaliza nafasi ya pili kwenye AFCON na Kouyate amesisitiza kwamba mchezaji mwenzake huyo angeshinda kama asingekuwa Mwaafrika.

LONDON, ENGLAND. STAA, Cheikhou Kouyate anaamini kwamba mchezaji mwenzake wa kimataifa wa Senegal, Sadio Mane amenyimwa tu tuzo ya Ballon d'Or kwa sababu ni Mwaafrika.

Mane alishika nafasi ya nne kwenye kinyang'anyiro cha tuzo hiyo iliyotolewa Jumatatu iliyopita huko Paris, Ufaransa na supastaa wa Barcelona na Argentina, Lionel Messi kuibuka mshindi akifuatiwa na Virgil van Dijk na Cristiano Ronaldo kwenye namba mbili na tatu. Mane alikuwa kwenye kiwango bora kabisa kwa mwaka 2019, akifunga mabao 54 kwenye klabu na timu yake ya taifa na aliisaidia Liverpool kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England.

Mane aliongoza Senegal kumaliza nafasi ya pili kwenye AFCON na Kouyate amesisitiza kwamba mchezaji mwenzake huyo angeshinda kama asingekuwa Mwaafrika.

Kiungo wa Crystal Palace, Kouyate alisema: “Kwangu mimi Ballon d’Or ni ya Sadio Mane, hakuna ubishi juu ya jambo hilo. Sikieni, kama Sadio angekuwa Mbrazili au Mzungu jambo hilo lisingekuwa mjadala. Angebeba tuzo hiyo moja kwa moja biola utata na hii si kwa sababu nacheza naye taifa moja, lakini hata watu wanaofuatilia soka wanaliona hilo.”

Mane aliweka nyavuni kwenye mchezo wa Merseyside derby wakati Liverpool walipoichapa Everton 5-2 kwenye Ligi Kuu England uwanjani Anfield juzi Jumatano.