Koscielny alipowashangaza wasiotaka kushangaa

Muktasari:

Arsenal inamlipa Pauni 90,000 kwa wiki na bado haikuwa hata na lengo ya kumtema.

SOKA la dunia ya kisasa. Soka la wanasoka wa kizazi hiki. Ukitaka kuondoka, unasusa tu. Unagoma au utatoweka tu. Unagomea timu, unawagomea mashabiki na hata wachezaji wenzako.

Haijalishi hata kama ni nahodha. Ndio namna mpya ya maisha ya wanasoka wa kisasa. Ni sahihi?

Laurent Koscielny ameingia kwenye kundi hilo. Ameshangaza kila mtu. Amewashangaza hata wasioshangaa. Hakuna aliyedhania kabisa kwamba kuna siku Koscielny ataamka na kulazimisha kuondoka Arsenal. Hakutaka kuheshimu hadhi yake klabuni hapo.

Hakutaka kuacha alama kubwa ya heshima kwa mashabiki na kutambulika kama mmoja kati ya wachezaji muhimu kwenye historia ya timu hiyo. Ameharibu kila kitu.

Amefanya uamuzi kwamba hataki tena kuichezea timu hiyo. Tazama umri wake ni miaka 33.

Arsenal inamlipa Pauni 90,000 kwa wiki na bado haikuwa hata na lengo ya kumtema.

Arsenal ilimheshimu kama nahodha wake, lakini hakulipa nafasi hilo. Amegoma kupanda ndege kuungana na wenzake huko kwenye kambi ya kujiandaa na msimu mpya Marekani.

Ndio uamuzi wake, kwamba ameshamaliza kuichezea Arsenal. Tabia hiyo ya hovyo, basi itamgharimu hata kwenye mshahara wake.

Hakikuwa kitendo kizuri kutoka kwa mchezaji mkomavu kama yeye, bila ya kujali kwamba yeye ni nahodha na wachezaji wenzake walikuwa wakimpa heshima kubwa. Jambo jingine bado ana mkataba na Arsenal. Bado anawajibika kwa majukumu yote kwa timu hiyo.

Koscielny alipaswa kupanda ndege na kuungana na wenzake kwenye kambi. Angeweza kutafuta namna nyingine ya kuishawishi Arsenal kumuuza aende anakotaka kwenda. Ni kweli ofa ya Lyon, Rennes na Bordeaux imemvuruga Koscielny na kulazimisha kuiacha Arsenal?

Haukuwa uamuzi sahihi. Kinachoelezwa kwenye ofa hizo tatu, Bordeaux ndio inayomzuzua beki huyo. Koscielny anapaswa kuheshimu mwaka wake mmoja uliobaki kwenye mkataba wake huko Emirates.

Hilo ni kwa sababu Arsenal ina haki ya kutaja bei inayotaka kwenye kumuuza mchezaji huyo. Arsenal inataka ilipwe Pauni 10 milioni kwenye mauzo ya mchezaji huyo. Koscielny anafahamu wazi Bordeaux haiwezi kulipa kiwango hicho cha pesa.

Tafsiri yake ya moja kwa moja anadhani Arsenal inagoma kumwaachia.

Hapo ndipo palipoanzia suala la kuamua kugoma, kuigomea timu kushinikiza imuuze tu. Koscielny amejisahau. Amesahau kwamba hata msimu uliopita hakuna kitu cha maana alichofanya kwenye kikosi hicho kutokana na muda mrefu kuwa nje ya uwanja kwa kuwa majeruhi.

Arsenal ilimvumilia na iliendelea kumlipa mshahara kamili bila ya kujali kwamba hakuwa anacheza. Imekuwa na heshima kwa nahodha wake. Lakini, hilo ndilo alilokuja kuilipa Koscielny. Alazimisha kuuzwa hata kama Arsenal haitaki kufanya hivyo. Huku ndiko alikofikia Koscielny.

Wengi wangemwelewa kama angekuwa analazimika kuhamia Real Madrid, Barcelona, Juvantus au Paris Saint-Germain. Au hata angekuwa analazimisha kuhamia Bayern Munich. Angeeleweka tu. Angetoa sababu tu kwamba anataka mataji, hakuna ambaye asingemwelewa. Tena kwa umri wake, hata Arsenal yenyewe ingemfungulia mlango wa kuondoka akatimize ndoto zake.

Lakini kuikataa Arsenal na kutaka kwenda Rennes au Bordeaux. Tena kwa kulazimisha, imewafanya wengi kushangaa. Kweli leo mchezaji anakataa kuichezea Arsenal na kuitaka Rennes au Bordeaux?

Hapo ndipo Koscielny anapowashangaza wengi, wanashindwa kumwelewa. Hata Arsenal yenyewe haimwelewi. Inachomwelewa ni kwamba itamkata mshahara na kuwapunguzia bajeti ya wiki mbili au tatu kwenye bili yake ya mishahara.

Nitaielewa Arsenal kama haitamuuza, kama itamvua unahodha na msimu ujao ikamweka kwenye benchi. Dawa ya moto ni moto, uamuzi bora kwa Arsenal ni kumuuza tu ili kuondoa virusi hatari kwenye kikosi chake.