Koscielny aleta kasheshe kubwa Emirates

Muktasari:

Staa huyo pia alionekana kutoridhishwa na klabu hiyo tangu aliporudi klabuni Desemba mwaka jana kutokana na majeraha ya muda mrefu huku pia akichezesha kwa dakika chache lakini pia hakuridhishwa na mwenendo wa klabu hiyo.

LONDON,ENGLAND.BUNDI ameanza kuunguruma mapema pale Arsenal. Nahodha wa timu, Laurent Koscielny amegoma kusafiri na timu hiyo kwa ajili ya ziara ya maandalizi ya msimu mpya Marekani na Arsenal tayari imemtunishia msuli staa huyo.

Koscielny, 33 atamaliza mkataba wake na Arsenal mwishoni mwa msimu ujao na anadaiwa amekuwa akisakwa na klabu za kwao Ufaransa, Bordeaux, Rennes na Lyon kwa ajili ya kwenda kumalizia maisha yake ya soka kwao Ufaransa.

“Tumeudhika sana na vitendo vya Laurent ambavyo ni kinyume cha maelekezo yetu yaliyo wazi. Tuna matumaini ya kumaliza suala hili na hatutatoa maelezo zaidi,” ilisema taarifa ya Arsenal katika tovuti yao kuhusu beki huyo wa Ufaransa.

Inadaiwa Bordeaux ipo tayari kumpa Koscielny aliyejiunga na Arsenal mwaka 2010 akitokea Lorient ya Ligi Daraja la Kwanza Ufaransa mkataba wa miaka mitatu na staa huyo amechoshwa na maisha ya Uingereza anataka kurudi nyumbani.

Kuelekea mwishoni mwa msimu uliopita, Arsenal na Koscielny zilikuwa katika mazungumzo ya kuongeza mwaka mmoja katika mkataba wake wa sasa na maongezi yaliendelea vizuri hadi pale Arsenal ilipochapwa na Chelsea katika pambano la fainali Kombe la Europa na matokeo hayo yakavuruga mipango ya Arsenal kifedha.

Staa huyo pia alionekana kutoridhishwa na klabu hiyo tangu aliporudi klabuni Desemba mwaka jana kutokana na majeraha ya muda mrefu huku pia akichezesha kwa dakika chache lakini pia hakuridhishwa na mwenendo wa klabu hiyo.

Wakati Koscielny akiamini kufuzu katika michuano ya Ligi ya Mabingwa kungeweza kuwa jambo zuri kwa upande wake na mambo hayakwenda sawa na kuanzia hapo aliamua ulikuwa wakati mzuri kwake kurudi nyumbani Ufaransa.

Wakati wachezaji wakianza kurudi katika klabu zao kutoka katika mapumziko ya majira ya baridi, huku klabu kadhaa zikionyesha nia ya kumchukua, staa huyo aliifahamisha Arsenal nia yake ya kuondoka na aliamini baada ya kuitumia klabu hiyo kwa miaka tisa wangeweza kumwacha huru aondoke bila ya kudai ada yoyote ya uhamisho.

Hata hivyo, Arsenal ilimkatalia maombi yake na ilimwambia wazi ilitazamiwa aheshimu mkataba wake na kuwa mchezaji muhimu kikosini kuelekea msimu ujao.

Inadaiwa Kocha wa Arsenal, Unai Emery alikuwa na furaha na kiwango cha Koscielny msimu wa 2018-19 huku tayari akiwa na matatizo katika safu yake ya ulinzi na kwa mtazamo wake angemruhusu beki huyo kuondoka kama angepata mchezaji muhimu katika nafasi yake.

Koscielny aliitaka Arsena imwachie aondoke bure dirisha la sasa ikiwa ni hisani yao kwake baada ya kuichezea timu hiyo kwa uaminifu mkubwa na kwa kipindi kirefu huku pia akidai Arsenal inaweza kumruhusu ikipokea ofa yoyote ile.

Staa huyo alimwambia Kocha Emery uso kwa uso siku ya Jumatano hatakwenda Marekani na timu kujiandaa na msimu mpya na inaeleweka kocha huyo kutoka Hispania alikasirika kupindukia.

Mkuu wa masuala ya soka wa Arsenal, Raul Sanllehi baadaye alimtumia ujumbe kwa simu staa huyo akielezea kusikitishwa kwake na kitendo cha kugomea kwenda Marekani huku akimkumbusha kwa kufanya hivyo alikuwa akivunja kipengele cha mkataba.

Koscielny alijibua alijibu akisisitiza msimamo wake wa kutokwenda Marekani na Alhamisi alipowasili katika uwanja wa mazoezi wa Arsenal, London Colney alithibitisha hatapanda ndege ya kwenda Marekani.

Kwa sasa staa huyo atatakiwa kufanya mazoezi na wachezaji ambao hawataenda Marekani, chipukizi wakati akisubiri hukumu yake. Maofisa wa Arsenal wamekerwa na hali hiyo hasa kwa mtazamo wa kisoka na kwa sasa nafasi ya ulinzi wa kati klabuni hapo imekuwa ikiwaumiza kichwa na wamekuwa wakisaka beki wa kati wa kuimarisha nafasi hiyo.