Kongamano la waigizaji kufanyika wiki ijayo jeshini

Muktasari:

Fisoo amesema mada zitakazotolea katika kongamano hilo zitawajengea uwezo waigizaji katika maeneo ya kujitangaza, kutengeneza kazi bora na wasanii kujua thamani yao.

Bodi ya filamu imeandaa kongamano litakalowasaidia wasanii kujithamini na kujitambua huku malengo yakiwa kuwafikia waigizaji nchi nzima. Bodi ya filamu nchini kwa kushirikiana na chama cha waigizaji Tanzania (TDFAA),wameandaa kongamano la waigizaji litakalokuwa na mada mbalimbali ikiwemo kujitambua na kujithamani.

Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu, Joyce Fisoo, amesema kongamano hilo litafanyika Aprili 15 mwaka huu katika Ukumbi wa Suma JKT.

Fisoo amesema mada zitakazotolea katika kongamano hilo zitawajengea uwezo waigizaji katika maeneo ya kujitangaza, kutengeneza kazi bora na wasanii kujua thamani yao.

"Tunataka ifike mahali msanii ajijue yeye ni nani na hata atakapofanya kazi iwe ya kulipwa au bure awe na mkataba wa kimaandishi badala ya sasa hivi baadhi wamekuwa wakitumiwa na watu kwa maslahi yao huku wao wakiwa hawana wanachofaidika," amesema. Jimmy Mafufu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa TDFAA, amesema wasanii wengi hawakuzaliwa na vipaji bali wamekuwa navyo kama wameviokota barabarani.

Kutokana na hilo Mafufu amesema wanaopata umaarufu wanakuwa malimbukeni, na kuona maisha ni kwenda baa kujenga heshima na kubadilisha magari kama nguo. "Wasanii wengi tunajuana maisha yetu sio kama yanavyoonekana machoni mwa watu na sio kwamba hatupati hela bali ulimbukeni wa ustaa unatusumbua, hivyo kongamano hili litatupa elimu namna ya kuishi maisha ya ustaa na kuheshimika na jamii," amesema.

Mwakilishi kutoka Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Denis Sweya maarufu kwa jina la Dino, amesema ni vema siku hiyo ya kongamano wasanii wakajitokeza bila kujali majina makubwa waliyonayo.

'Ni kawaida wasanii wanaojiita wakubwa hapa nchini kunapotokea fursa ya makongamano kama haya kutojitokeza bila kujua huko kuna elimu ambayo huenda wangetumia hela kuipata,"amesema Dino.