Kona hizi za Carlinhos Lamine atafunga sana

YANGA imepata ushindi wa pili mfululizo katika mechi zake mbili za ugenini huku beki Lamine Moro akiendelea kuipa ushindi wa pili ndani ya mechi tatu.

Wakati Moro aking’aa kwa kuipa pointi tatu kwa mara ya pili timu yake lakini nyuma ya mabao hayo mawili utamu ni kwamba yametengenezwa na kiungo mmoja Carlos Carlinhos akitumia ufundi wa mipira yake mikali ya kona.

Itakumbukwa Moro alifunga bao lake la kwanza dhidi ya Mbeya City akifunga kwa kichwa akitumia kona ya Carlinhos na juzi pia akawafunga Mtibwa Sugar pale Uwanja wa Jamhuri, akitumia tena kona ya kiungo huyohuyo, lakini mara hii akiumalizia mpira kwa mguu.

Bao la mpira wa adhabu halikutokea kwa bahati mbaya, kwa mujibu wa kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi.

Carlinhos ambaye tangu awasili nchini amekuwa katika wakati mgumu kuwa fiti kutokana na kushindwa kuzoea haraka vyakula vya Kitanzania kabla ya kupatiwa mpishi maalum hivyo karibuni, hakutarajiwa kuanza mechi kwenye uwanja usio na viwango wa Jamhuri Morogoro juzi.

Lakini mpango sahihi wa kiufundi kutoka katika benchi la ufundi la Yanga, uliifanikisha timu hiyo kupata pointi tatu baada ya kuamua kumuanzisha kiungo huyo mtaalamu wa mapigo ya mipira iliyokufa.

Mwambusi alisema walimuanzisha Carlinhos pembeni kwa sababu walijua eneo la kati litakuwa limejaa watu lakini walihitaji kutumia mipira ya adhabu ndogo katika uwanja huo usio na eneo zuri la kuchezea na ambao Bodi ya Ligi iliufungia kutumika kwa mechi za ligi muda mfupi baada ya mechi hiyo kumalizika.

Mazingira ya uwanja hayakuwa mazuri kwa timu zote, jambo lililozuia mchezo wa kuvutia.

Timu zililazimika kupiga mipira mirefu na kuikimbiza.

Mtibwa ambayo imekuwa ngumu kwenye uwanja wake huo wa nyumbani na ambayo iliwavimbia mabingwa wa ligi hiyo Simba katika sare ya 1-1 wiki iliyopita, ilishindwa kuboresha rekodi yake nzuri ya kutofungwa na Yanga Jamhuri tangu 2015, shukrani kwa mbinu ya benchi la ufundi la Yanga ya kutumia mipira iliyokufa.