Kompany aondoka Manchester City,aenda kumkaba Mbwana Samatta

Muktasari:

Kompany, mwenye umri wa miaka 33 sasa ataondoka Etihad na kurudi katika klabu yake ya zamani ya Anderlecht, ambapo anakwenda kuwa kocha mchezaji.

Manchester,England.CHENYE mwanzo hakikosi mwisho. Lakini, kila mtu angependa kuwa na mwisho kama wa Vincent Kompany huko kwenye kikosi cha Manchester City.

Klabu hiyo imetangaza haitakuwa tena na huduma ya nahodha wake huyo msimu ujao baada ya kukipiga kwenye kikosi hicho kwa miaka 11. Lakini, Kompany amefunga ukurasa wake wa mwisho kuhusu Man City kwa mafanikio makubwa akibeba mataji manne katika msimu wake wa mwisho, akianzia lile la Ngao ya Jamii, kisha Kombe la Ligi, Ligi Kuu England na kumalizia na Kombe la FA.

Kompany, mwenye umri wa miaka 33 sasa ataondoka Etihad na kurudi katika klabu yake ya zamani ya Anderlecht, ambapo anakwenda kuwa kocha mchezaji.

Beki huyo Mbelgiji anarudi kwao kujiunga na klabu yake ya zamani Anderlecht, mahali ambako atakwenda kufanya kazi ya kumkaba straika wa Genk, Mbwana Samatta kama ataendelea kubaki kwenye kikosi hicho kwa msimu ujao.

Katika barua yake ya wazi aliyoandika kwenye ukurasa wake wa Facebook, Kompany aliandika hivi: “Nimeamua kuwa mtulivu kwa yaliyopita, lakini nikiwa na hamu na yajayo. Kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo, nimekubali kuwa kocha mchezaji wa RSC Anderlecht. Timu bora kabisa ya Ubelgiji.

“Pengine hili litawashangaza wengi. Ni uamuzi sahihi kabisa niliwahi kuufanya. Nikiwa mwanasoka, nilizaliwa na kukulia RSC Anderlecht. Tangu nikiwa na umri wa miaka sita, nimekuwa mmoja wa waliotokea kwenye klabu hiyo. Wana historia ya mataji 34, ni bora hakuna mwingine.”

Kompany ameshinda mataji manne ya Ligi Kuu England tangu alipojiunga na Man City mwaka 2008, huku mataji mengine aliyobeba ni Kombe la FA mara mbili, Kombe la Ligi mara nne na Ngao ya Jamii mara mbili.

Amecheza mechi 360 katika klabu hiyo, akifunga mabao 20, la mwisho likiwamo lile la shuti muhimu dhidi ya Leicester City lililoisaidia timu hiyo kusogelea kwenye ubingwa wa ligi na kufanikiwa kuutetea.

Lakini misimu minne ya mwisho ya Mbelgiji huyo huko Etihad imekuwa ya majanga mengi ya kuwa na majeraha hivyo kupunguza mchango wake kwenye timu.

“Nilikwenda kwenye uwanja wao wa mazoezi mwaka jana nilikiwa kwenye majukumu ya timu ya taifa. Nilikwenda kuwasalimia tu,” alisema Kompany.

“Marc Coucke, mwenyekiti na mkurugenzi wa soka, Michael Verschueren waliniomba ushauri kuhusiana na hali ngumu iliyokuwa ikipitia klabu. Niliwapa ushauri wangu na kusikia mawazo yao na nimeona mipango mizuri ya kurudi kuwa namba moja.

“Niliwapa ofa ya kuwasaidia. Baadaye, mkurugenzi mpya wa ufundi, Frank Arnesen alipokuja walifanya mambo kadhaa ya kiufundi ili kujenga kikosi bora cha kuvutia na kushambulia. RSCA imekuwa na utamaduni wa kutengeneza vijana mahiri.”

Kompany alimaliza kwa kusema hataki kusema kwaheri, akiamini ataonana tena baadaye na mashabiki wa Man City.

Mwenyekiti wa Man City, Khaldoon Al Mubarak alisema kuna wachangiaji wengi sana muhimu waliopata kutokea kwenye kikosi hicho, lakini bila ya ubishi hakuna mchezaji muhimu zaidi kupita Kompany.