Kombinesheni matata za makocha, wachezaji vikosini

LONDON, ENGLAND. SOKA lina mambo yake. Asikwambie mtu kwenye soka kuna mambo mengi ikiwamo mastaa waliowahi kucheza chini ya makocha ambao wengi watakuwa wamesahau au hawafahamu kama walishawahi kuwa kwenye timu moja.

Rafa Benitez na Cristiano Ronaldo (Real Madrid)

Rafa Benitez ambaye aliwahi kuzinoa timu nyingi ikiwamo Newcastle United, aliwahi kumnoa pia Cristiano Ronaldo. Katika msimu wa 2015/16 kocha huyo Mhispaniola alipata nafasi ya kuinoa Real Madrid, mahali ambako alikutana na Ronaldo, ambaye alicheza mechi 24 chini yake. Katika mechi hizo, Ronaldo alionyesha kiwango bora akifunga mabao 25 na kuasisti mara nane na kufanya kombinesheni yao kuleta matunda bora.

Arsene Wenger na Glenn Hoddle (Monaco)

Hiki ni kitu ambacho usingeweza kukifikiria kabisa, lakini ndio hivyo, Hoddle aliwahi kuwa chini ya kocha Arsene Wenger. Wawili hao walikutana mwishoni mwa miaka ya 80 na mwanzoni mwa miaka ya 90 huko Monaco. Chini ya Wenger, kiungo Hoddle alipewa uhuru wa kucheza kwa kadri anavyoweza, ambapo alitumikia timu ya kocha huyo Mfaransa mara 76 na kufunga mabao 27 akitokea kwenye sehemu ya kiungo.

Roy Hodgson na Roberto Carlos (Inter Milan)

Ndio hivyo, Roy Hodgson aliwahi kumnoa mchezaji mwenye kipaji kikubwa cha soka kama vile Roberto Carlos. Wawili hao walikuwa pamoja huko Inter Milan. Kocha huyo Mwingereza, Hodgson alichukua mikoba ya kuinoa klabu hiyo ya Italia kati ya mwaka 1995 na 1997, ambapo beki huyo Mbrazili alicheza mechi 23 chini yake. Roberto Carlos, ambaye baadate alikwenda kushinda ubingwa wa Kombe la Dunia akiwa na kikosi cha Brazil, chini ya Hodgson alifunga mabao manne. kocha huyo kwa sasa anainoa Crystal Palace.

Diego Simeone na Alexis Sanchez (River Plate)

Huu ni uhusiano mwingine wa mchezaji na kocha ambao ni ngumu kukumbukwa kwamba uliwahi kutokea. Lakini, habari ndiyo hiyo, Alexis Sanchez aliwahi kuwa chini ya kocha Simeone. Wawili hao wangekutana kwa sasa huko Atletico Madrid ingekuwa balaa zaidi, lakini walikutana River Plate huko Argentina. Sanchez alicheza mechi 15 chini ya kocha Simeone mwaka 2008 na alifunga bao moja tu. Badaa ya hapo, Sanchez alicheza timu kibao kubw za Ulaya, ikiwamo Barcelona, Arsenal, Manchester United na sasa Inter Milan.

Sam Allardyce na Fernando Hierro (Bolton)

Allardyce na Hierro ni mastaa wawili wa soka waliowahi kuwa kwenye timu moja. Hierro alikuwa gwiji Real Madrid alikofunga mabao 124 huku akiwa beki matata kabisa kwenye kufunga mabao. Lakini, katika nyakati za mwisho za maisha yake ya soka alikwenda kukipiga Bolton, mahali ambako alikwenda kukutana na kocha Allardyce katika msimu wa 2004/05. Chini ya kocha Big Sam, Hierro alicheza mechi 32 na kufunga bao moja tu, akishindwa kuonyesha makali yake aliyokuwa nayo huko Bernabeu.

Sir Alex Ferguson na Gerard Pique (Man United)

Huu ni uhusiano mwingine bora kabisa kwenye mchezo wa soka. Ni rahisi kukumbuka kwamba beki Pique aliwahi kukipiga kwenye Ligi Kuu England na alifanya hivyo kupitia kikosi cha Manchester United kilichokuwa chini ya Sir Alex Furguson. Mhispaniola huyo kwa sasa anakipiga Barcelona na panga pangua alikuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha timu ya taifa ya Hispania. Chini ya Sir Alex, beki Pique alicheza mechi 23 kwa kipindi cha miaka minne kati ya 2004 na 2008 kabla ya kurudi kwenye klabu yake ya zamani iliyomkuza Barcelona.

Roberto Mancini na Kieran Trippier (Man City)

Hii utashangaa kuwamo kwenye orodha hii kwa sababu Trippier hakuwahi kabisa kucheza chini ya Mancini, lakini alikulia huko Manchester City wakati huo Mtaliano huyo alikuwa bosi Etihad. Beki huyo Mwingereza kwa sasa anakipiga kwenye kikosi cha Atletico Madrid, lakini alitajwa na Mancini kwenye kikosi chake kilichokwenda kwenye ziada ya kuajiandaa na msimu mpya mwaka 2010. Jambo hilo linawafanya Trippier na Mancini kuhusiana kwa namna fulani kwenye moja ya kazi zao za mchezo wa soka.

Jose Mourinho na Fabinho (Real Madrid)

Kiraka wa Liverpool, Fabinho aliwahi kucheza kwa muda mfupi kwenye kikosi cha Real Madrid katika msimu wa 2012/13, lakini kwa bahati mbaya hakupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza. Alicheza kikosi B mara kibao huku fursa pekee ya kuichezea timu A, ilikuwa pale kocha Jose Mourinho alipomwita kwenye mechi ya mwisho na kumchezesha kwa dakika 14 tu. Kwa sasa, Mbrazili Fabinho anakipiga huko Liverpool, akitamba kwa kiwango bora kabisa baada ya kunasa kwa Pauni 54 milioni kutoka AS Monaco.

Nigel Pearson na Harry Kane (Leicester City)

Harry Kane ni straika matata kabisa linapokuja suala la kutupia mipira nyavuni na sasa anafanya kazi yake hiyo bora kabisa ya kuwatesa makipa kwenye kikosi cha Tottenham Hotspur. Hata hivyo, kabla ya kuwa staa mkubwa huko Spurs na timu ya taifa ya England, Kane aliwahi kuwa chini ya kocha Chris Hughton huko Norwich City, kisha alikwenda kunolewa na Nigel Pearson alipokwenda kwa mkopo Leicester City. Kane aliifungia Leicester City mabao mawili katika mechi 15 alizochezea miamba hiyo ya King Power.

Sir Bobby Robson na Ronaldo Nazario

(Barcelona)

Ronaldo Nazario alikuja kuwa gwiji huko Real Madrid na imekuwa ngumu kwa wengi kukumbuka kwamba aliwahi kuichezea Barcelona, ambao ni mahasimu wakubwa wa miamba hiyo ya La Liga kwenye El Clasico. Ronaldo alikuwa kwenye kikosi cha Nou Camp msimu wa 1996/97 chini ya kocha Bobby Robson. Fowadi huyo Mbrazili alifunga mabao 47 katika mechi 49 alizocheza chini ya Robson. Ronaldo pia aliasisti mara 12 na kutoa huduma bora kabisa kwa Robson.

Pep Guardiola na Ibrahim Afellay (Barcelona)

Ndo hivyo, Afellay aliwahi kuichezea Barcelona katika kipindi ambacho walikuwa wakicheza soka matata kabisa ndani ya uwanja. Lakini, baadaye Mdachi huyo alitimkia zake Stoke City na kisha Olympiacos. Akiwa Barcelona, alicheza chini ya Guardiola - ambapo alipangwa kwenye mechi 33 na kufunga mabao mawili na kuasisti mara moja. Hii ni moja ya ushirikiano wa kikazi baina ya kocha na mchezaji ambao wengi wamekuwa hawaufahamu. Guardiola baadaye alikuja kwenye soka la England na sasa anainoa Manchester City.