Koeman akubali yaishe

BARCELONA, HISPANIA. KOCHA wa Barcelona, Ronald Koeman amesema hakuweza kupata asilimia kubwa ya wachezaji ambao alikuwa anahitaji kuwatumia kwenye kikosi kwa msimu huu, lakini anaamini wachezaji waliomo kwenye timu yake ni wazuri na ana furahi kuwa nao.

Barca ilishindwa kufanya usajili huo kutokana klabu hiyo kuyumba kiuchumi kulikosababishwa na janga la virusi vya corona hivyo inataka kuelekezea nguvu zake katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ikiamini mpaka wakati huo tayari hali yao itakuwa nzuri kiasi.

Barca imeachana na wachezaji wake wanne katika dirisha liliopita ikiwa ni pamoja na Luis Suarez, Arthur, Ivan Rakitic na Arturo Vidal na ikawasainisha Miralem Pjanic, Sergino Dest na makinda Trincao, Pedri na Matheus Fernandes.

“Kikosi kipo sawa sawa na nina furaha kuwa na wachezaji hawa, tulijaribu kufanya maboresho katika baadhi ya maeneo, lakini kuna baadhi ya wachezaji hatukufanikiwa kuwapata na hii ilitokana hali ya kiuchumi ya klabu kwahiyo kulikuwa hakuna namna, tunapaswa tukubaliane nayo na kuanza kufanya kazi,” alisema.

Barcelona ilitangaza kuwa imepata hasara ya Pauni 87 milioni sambamba na kupungua kwa zaidi ya Pauni 184 milioni kwenye mapato yao.

Koeman alikuwa anahitaji zaidi saini ya winga wa Uholanzi na Olmpique Lyon, Memphis Depay lakini dili lilifeli na badala yake ameamua kumtumia Ansu Fati ambaye ameonekana kuonesha kiwango kikubwa na kuwa kipenzi cha mashabiki wa Barca.

Fati amefunga mabao matatu mpaka sasa pia amekiwasha ile mbaya hadi kwenye timu ya Taifa ya Hispania.

“Kucheza mechi tatu mfululizo kwenye Ligi Kuu, Hispania ni ishara nzuri.”