Kocha wa riadha kampa mchongo Filbert Bayi

Muktasari:

  • Katika ziara yake kwenye Taasisi za Filbert Bayi, Thandi alitembelea shule za mwanariadha huyo zilipo Kibaha Mkuza na Kimara, viwanja vya michezo katika shule hizo, Hospitali ya Filbert Bayi na uwanja wa ndani wa michezo wa mwanariadha huyo.

BALOZI wa kwanza wa Afrika Kusini nchini, Thandi Lubaje-Rankoe ameshangazwa na uwekezaji wa mwanariadha mkongwe nchini, Filbert Bayi na kuwausia vijana wanaosoma kwenye shule za nguli huyo wa riadha kufuata nyayo za mwanariadha huyo.

Thandi ambaye aliteuliwa na Rais wa Kwanza wa Afrika Kusini, Nelson Mandela kuwa balozi wa Afrika Kusini nchini baada ya nchi hiyo kuondokana na ubuguzi wa rangi alimtembelea nyota huyo mkongwe wa riadha baada ya kupata taarifa zake kupitia kwa aliyekuwa kocha binafsi wa Bayi, Ron Davis.

“Naikumbuka Tanzania namna ilivyotusaidia kupigania uhuru wetu, nakumbuka namna Rais Mandela alivyoniteua nije kuwa balozi wake mara tu baada ya uhuru na kuishi hapa kwa amani, upendo na ukarimu,” alisema Thandi katika hotuba yake kwa wanafunzi wa shule hiyo.

Thandi ambaye amekuja nchini kwa mapumziko mafupi, alisema kuja kwake Tanzania kwa mara nyingine ni kama amerudi nyumbani kwani nchi hii ni nchi yake ya pili baada ya Afrika Kusini na hakusita alipoombwa amtembelee Bayi ambaye ni mwanariadha mwenye historia sio tu Tanzania bali duniani .

Katika ziara yake kwenye Taasisi za Filbert Bayi, Thandi alitembelea shule za mwanariadha huyo zilipo Kibaha Mkuza na Kimara, viwanja vya michezo katika shule hizo, Hospitali ya Filbert Bayi na uwanja wa ndani wa michezo wa mwanariadha huyo.

“Bayi amefanya mambo makubwa, nilipopata habari zake na mwaliko wa kumtembelea, nilienda ‘google’ nikamtafuta, ni mtu ambaye anastahili pongezi, lakini pia vijana mliobahatika kusoma hapa jifunzeni kupitia yeye,” alisema.

Akizungumzia ujio wa Thandi, Bayi alisema balozi huyo mstaafu alipata taarifa zake kupitia kwa Kocha Ron Davis aliyewahi kuwa karibu na Rais wa Kwanza wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.

Kwa mujibu wa Bayi, Ron Davis ambaye amewahi pia kuinoa timu ya taifa iliyoiletea nchi medali mbili za Olimpiki ya 1980 ndiye alimuunganisha Thandi kwake.

“Alisema atakuja kutembelea Taasisi za Filbert Bayi, hilo lilikuwa jambo jema kwetu na hata kwa vijana wanaosoma hapa ambao wapo wat akaohitaji kufuata nyayo zake, kwani Thandi alikuwa ni miongoni mwa watu maarufu katika utawala wa Mandela,” alisema.