Kocha wa Harambee Stars aanza mikakati ya Afcon

Muktasari:

Aidha aliongeza kuwa kama atatokea mchezaji mwingine akamfurahisha huku ligi ikiwa inakaribia ukingoni, basi atamwitia nafasi kwenye kikosi chake huku akimtema ambaye hatakuwa amemridhisha kabisa.

KOCHA wa timu ya taifa Harambee Stars alianza maandalizi ya timu yake  kwa ajili ya michuano ya AFCON 2019 kwa kutangaza kuwa atawachuja wachezaji wanne watakaofeli kumfurahisha kufikia wiki ijayo.

Migne aliingia kambini Jumatatu na baadhi ya wachezaji wachache aliowataja kwenye listi yake ya wachezaji 30.

Akifunguka, kocha huyo Mfaransa alisema kuwa kikao hicho na kuendelea kilikuwa cha kugeji kiwango cha fitinesi cha wachezaji aliowaita kambini.

Aidha aliongeza kuwa kama atatokea mchezaji mwingine akamfurahisha huku ligi ikiwa inakaribia ukingoni, basi atamwitia nafasi kwenye kikosi chake huku akimtema ambaye hatakuwa amemridhisha kabisa.

“Tunahitaji kuboresha utimamu wa wachezaji ili kuwa na balansi nzuri kwenye timu, Na labda niseme hivi mimi ni mhalisia, kama akitokea mchezaji ambaye sijamtaja na akanipendeza na kiwango, mara moja nitamwita kwenye timu  kabla tusafiri kwenda Ufaransa. Na wiki ijayo nitaipunguza kikosi hadi kubakia wachezaji 26 kwa kutegema nitakachokuwa nimekiona kwenye kambi hii” alisema Migne.

Baada ya msimu wa ligi kuu kutamatika, Stars wataabiri ndege na kusafiri hadi Paris Ufaransa watakakodunga kambi ya siku 19 kwenye  viwanja vya makao makuu ya Shirikisho la soka Ufaransa, Marcoussis Cedex.

Baada ya kambi hiyo, Stars watasafiri moja kwa moja hadi Cairo, Misri Juni 19, tayari kwa dimba la AFCON 2019 itakayoanza siku tatu badaye.